Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Utumishi na Utawala bora, Seleman Jafo amefunguka na kusema kuwa katika bajeti ya mwaka 2017/2018 inakwenda kutekeleza ulipwaji wa madeni ya walimu ambao wamekuwa wakidai malimbikizo yao kwa serikali.
Jafo amesema hayo bungeni leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, Mussa Sima ambaye alitaka kufahamu ni kama serikali itakuwa tayari kulipa malimbikizo ya mshahara kwa watumishi ambao walistahili kupanda madaraja mwaka jana lakini walishindwa kupanda kutokana na zoezi la ukaguzi wa vyeti vyeti. Akitolea maelezo jambo hilo Naibu Waziri Jafo anasema kuwa serikali itawalipa watumishi wote stahiki zao.
“Mhe. Naibu Spika tukifanya rejea ya siku mbili tatu hapo nyuma, Waziri wa Utumishi na Menenjimenti ya Umma alitoa maelekezo hapa kwamba katika hoja ya bajeti yetu kuu iliyokuwa inapita watu walikuwa wanasema kwanini nyongeza ya mshahara kundi hili halipo, na tukumbuke Mhe. Rais alizungumza wazi siku ya Mei Mosi kwa hiyo jambo hili limezingatiwa katika bajeti hii tunayokwenda nayo hivi sasa, ndiyo maana hata juzi Waziri wa Utumishi wa Umma alikuwa anatoa maelekezo kuwa kuna fedha na zaidi itakwenda kushugulikia jambo hilo” alisema Jafo
Seleman Jafo anasema kuwa suala la watumishi kupanda madaraja lilikwama kutokana na zoezi la uhakiki na ukaguzi wa watumishi hewa na vyeti feki na kusema sasa sauala hilo limewekewa utaratibu mzuri hivyo watumishi wataanza kupanda madaraja na kupata stahiki zao.
“Naomba nifanye rejea Waziri wetu wa Utumishi wa Umma alipozungumza wazi kwamba suala la kupanda madaraja sasa limewekewa utaratibu maalum na mzuri kuwa kila mtu sasa atapata stahiki yake kadili inavyotakiwa na ilivyokusudiwa” alisisitiza Jafo