Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 21 Julai, 2017 amezindua ujenzi wa barabara za Kibondo – Nyakanazi na Kidahwe – Kasulu, na amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Kigoma kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kukamilisha ujenzi wa barabara yote ya Kidahwe – Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 310 kama alivyoahidi.
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kasulu – Kibondo – Kakonko yenye urefu wa takribani kilometa 200 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa.
Taarifa ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa imeeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kibondo – Nyakanazi yenye urefu wa kilometa 50 utagharimu Shilingi Bilioni 48.57 na barabara ya Kidahwe – Kasulu yenye urefu wa kilometa 63 utagharimu Shilingi Bilioni 66.331, fedha zote zinatolewa na Serikali ya Tanzania na miradi yote miwili imepangwa kukamilika ifikapo Septemba 2018.
Akizungumza na wananchi katika sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara hizo na wananchi waliokuwa wakisimamisha msafara wake katika vijiji vya Kakonko, Kibondo, Kifura, Busunzu, Mkuyuni, Mvugwe, Makere na Kasulu Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amesema Serikali imedhamiria kuimarisha barabara za ukanda wa magharibi ili kuchochea uchumi wa wananchi na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani na ukanda huo.
Hata hivyo Mhe. Dkt. Magufuli ametaka wananchi ambao wamejenga nyumba katika hifadhi ya barabara ambayo ni meta 22.5 kila upande waondoe nyumba hizo kwa hiari kwa kuwa Serikali haitalipa fidia yoyote kwa waliojenga kwenye hifadh ya barabara.
Kuhusu tatizo la uhaba wa maji ambalo wananchi wameomba Serikali iwasaidie, Mhe. Rais Magufuli ameahidi kumtuma Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge kwenda katika maeneo yote yenye matatizo ya maji ili kupata ufumbuzi.
Katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Kasulu Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la wananchi kupatiwa sehemu ndogo ya hifadhi ya Kagerankanda ambayo wanaitumia kuzalisha mazao ya chakula na amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga kupima eneo hilo na kuwagawia wananchi.
Akiwa njiani kuelekea Kigoma Mjini Mhe. Rais Magufuli amesimamishwa na wananchi wa Kibwigwa, Buhigwe na Manyovu, na amewahakikishia kuwa barabara ya Kasulu – Manyovu yenye kilometa 42 itajengwa kwa kiwango cha lami.
Katika ziara ya leo Mhe. Rais Magufuli ameongozana pia na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Prof. Joyce Ndalichako, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma.
Kesho tarehe 22 Julai, 2017 Mhe. Rais Magufuli ataendelea na ziara yake hapa Mkoani Kigoma ambapo atazindua ujenzi wa mradi mkubwa wa usambazaji maji katika mji wa Kigoma na kuzungumza na wananchi Mjini Kigoma.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kigoma
21 Julai, 2017
0 comments :
Post a Comment