Mkuu wa habari na mawasiliano wa klabu ya Simba, Haji Sunday Manara ameishukuru kamati ya nidhamu ya shirikisho la soka Tanzania (TFF) kwa kumuondolea adhabu aliyokuwa amepewa ya kufungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa muda wa mwaka mmoja.
Manara alikuwa amefungiwa na TFF tangu Aprili 23, mwaka huu kwa makosa ya lugha chafu kwa viongozi wa TFF adhabu iliyoambatana na faini ya shilingi milioni tisa, lakini jana (Julai 17, 2017) kamati ya nidhamu chini ya mwenyekiti wake Tarimba Abbas ilimfutia adhabu hiyo kutokana na maombi aliyokuwa ameyatuma ya kupitiwa upya adhabu hiyo.
Katika taarifa yake aliyoitoa baada ya kuondolewa adhabu hiyo, Manara amesema adhabu hiyo ilikuwa inaiumiza klabu yake ya Simba na kuiondolea haki yake muhimu, ya kuwapa habari kwa wakati watanzania juu ya kinachoendelea ndani ya klabu hiyo.
“Hakika hawa wamesikia kilio cha wengi, na kilio cha wengi kina nguvu ya Mungu Mwenyezi, Shukran kwa Mola kwa kuwapa nguvu hii kina Tarimba na wenzake. Niwashukuru pia viongozi wa TFF kwa utashi wao kwenye hili”. Amesema Manara
Pia Manara amesema hataki kurudi kwenye mambo yaliyotokea nyuma, na kuwataka wadau wote kuungana na kusonga mbele kwa manufaa ya mpira wa miguu nchini, huku akiahidi kufanya kazi yake kwa ueledi na kuzingatia miiko ya michezo.
“Sitapenda kufukua makaburi, yatupasa sote tusonge mbele, hakuna aliyeshinda, umeshinda mchezo wa soka” Amesisitiza Manara
0 comments :
Post a Comment