Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kupitia Baraza la Mitihani (NECTA), imekamilisha kazi ya kupitia vyeti vya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Vyeti hivyo vilipelekwa wizarani na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ajili ya kuhakiki uhalali wa wagombea, na wale ambao elimu zao zitaonekana hazina dosari, wataruhusiwa kuendelea na mchakato.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Uchaguzi, Mohamed Mchengerwa, amesema tayari wizara hiyo imekwishampa taarifa ya kumaliza kazi ya uhakiki wa vyeti hivyo na kwamba wakati wowote kuanzia leo atakabidhiwa taarifa hiyo.
“Wizara imeshamaliza kazi, na tayari wamenitaarifu, na kazi hiyo nimeachiwa mimi kutokana na uzoefu wangu, kwahiyo wakati wowote kama siyo leo, basi kesho, tutakuwa tumepata taarifa na tutatoa orodha mpya bila kumuonea mtu,” amesema Mchengerwa wakati akizungumza na Azam TV.
Mchengerwa ambaye ni miongoni mwa wajumbe wapya kwenye kamati hiyo, amewataka wagombea wote wawe na imani na kamati hiyo kwani wote walioteuliwa hivi sasa ni wanasheria na wanafanya kazi kwa kuzingatia haki na ueledi wa hali ya juu na kwamba hawamuwakilishi mgombea yeyote.
Mbunge huyo wa Rufiji amesema yeye mwenyewe ana uzoefu wa kutosha wa kufanya kazi za uamuzi na amewahi kuwa hakimu, hivyo kazi hiyo aliyopewa na TFF haiwezi kumshinda huku akisisitiza kuwa wote waliokatwa kwa kutowasilisha vyeti, ni kweli hawakuwasilisha vyeti, jambo ambalo ni kinyume na kanuni.
“Tumeingia pale tumekuta majina yamekatwa hovyo hovyo bila sababu, watu kama Ally Mayay alikuwa amekatwa, Wallace Karia amekatwa.. wote tumewarudisha maana walikatwa bila kuzingatia kanuni,” amesema Mchengerw