Matokeo ya mtihani wa kidato cha sita yametoka huku kama kawaida kukiwa na shule kumi zilizofanya vizuri, na kumi zilizofanya vibaya.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa(Necta), Dk Charles Msonde amezitaja shule kumi zilizofanya vibaya na sehemu zinakotoka kwenye mabano kuwa ni Chasasa (Pemba), Kiembesamaki (Unguja), Mwenyeheri Anuarite (Dar), Ben Bella (Unguja) na Meta ya Mbeya.
Nyingine zilizoshika mkia katika orodha hiyo ni Mlima Mbeya (Mbeya), Njombe (Njombe), Al-Ihsan Girls (Unguja), St Vincent ya Tabora na Hagafilo (Njombe).
Wakizungumzia matokeo mabaya ya shule zao, baadhi ya walimu walisema matayarisho duni, kupokea wanafunzi waliofanya vibaya kidato cha nne, ndiko kulikowaponza.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Hagafilo mkoani Njombe, Castory Kayombo alisema walitarajia matokeo hayo kutokana na aina ya wanafunzi waliokuwa wamewapokea.
“Tulipokea wanafunzi ambao walikuwa hawajiwezi darasani, wengi walikuwa na daraja la nne kwenye matokeo ya kidato cha nne, hivyo licha ya kujitahidi kuwafundisha, ndio tumeambulia matokeo hayo,” alisema.
Hata hivyo, alisema wataendelea na mikakati yao ya kufanya vizuri ili mwakani, wasipate matokeo ya mwisho kama ilivyo mwaka huu.
Mmoja wa walimu wa Shule ya Sekondari Meta, jijini Mbeya Neema Matonya alisema bado hawajapata matokeo hayo na kwamba, kwa sasa hawawezi kuzungumza lolote.
“Bado hatujayapata hayo matokeo kwa hiyo hatuwezi kuzungumza lolote,”alisema



0 comments :
Post a Comment