Chama Kikuu Cha Upinzani Tanzania CHADEMA.....Kwenda Mahakamani Kudai Haki Ya kikatiba Yakufanya Mikutano Ya Hadhara


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kinajipanga kwenda Mahakama Kuu kudai haki ya mikutano iliyopigwa marufuku kwa agizo la Rais John Magufuli.


Aidha, chama hicho kimesisitiza kuwa mikutano ya siasa ni halali kikatiba.

Akizungumza na gazeti la  Nipashe juzi mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa chama hicho na wanahabari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema mikutano ni haki ya msingi ambayo lazima waitafute.

Nipashe ilitaka kujua hatua ambayo Chadema imefika kufuatia kauli ya Julai 16, mwaka huu, ya Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Lowassa, ambaye alidokeza suala hilo.

Akiwa nchini Kenya, Lowassa alisema chama hicho kitakwenda mahakamani kudai haki ya mikutano, lakini bila kutaja siku wala hatua iliyofikiwa na Chadema katika jambo hilo.

“Ni kweli tutakwenda mahakamani, kwa sasa tupo kwenye mchakato,” alisema na alipoulizwa ni lini alisema, “hivi karibuni."
"Subiri mtaona... mikutano ni haki ya chama chochote cha kisiasa na lipo kisheria, hivyo tutakwenda kulidai.”

Kanuni za maadili ya Vyama vya Siasa sura ya 258 za mwaka 2007 sehemu ya pili, kifungu cha nne kimetoa haki ya mkusanyiko kwa vyama hivyo nchini.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kutoa elimu ya uraia na elimu ya uchaguzi kwa wananchi kwa kufuata sheria na kanuni za nchi.

Haki nyingine ni kutoa maoni ya kisiasa kadri itakavyoona inafaa ili kutekeleza sera zake, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa, Katiba ya Jamhuri na Zanzibar.

Nyingine ni kujadili na kushindanisha sera zake na zile za chama cha siasa kingine kwa lengo la kutaka kukubalika na wananchi, kuwa na uhuru wa kutafuta wanachama na kama ni wakati wa kampeni basi kuwe na uhuru wa kutafuta kuugwa mkono na wapiga kura.

Haki nyingine ni kila chama cha siasa kuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa.

RAIS ALIPIGA
Juni mwaka jana, Rais Magufuli alipiga marufuku shughuli za kisiasa hadi mwaka 2020, hasa maandamano na mikutano ya hadhara.

Juni 24, mwaka jana, wabunge Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoa tamko Bungeni kupinga agizo hilo na kueleza kuwa uhalali wa kazi za siasa umetolewa na Katiba na sheria namna 5 ya mwaka 1992.

Mbowe wakati huo alieleza mambo 16 yanayowapa uhalali wa kufanya kazi ya siasa nchini, ikiwamo kuwa ni kazi kama zilivyo nyingine na kwamba imeruhusiwa na sheria za nchi.

“Ukawa hatutakubaliana na hali hii, hili ni tamko la hatari kwa demokrasia, utawala wa sheria, haki za binadamu,” alisema Mbowe.

Katika tamko hilo, Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa hali ya kufanya siasa haiwezi kuwa miliki ya serikali, wabunge na madiwani pekee bali vyama vyote.

Kufuatia agizo hilo, Agosti 25, mwaka jana, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salim Mwalimu na viongozi wengine, walikamatwa na polisi mkoani Shinyanga.

Agosti 30, mwaka jana, Lowassa, Mbowe, Johna Mnyika na Katibu Mkuu wa chama hicho Taifa, Dk. Vicent Mashinji walikamatwa na polisi wakati wakiwa kwenye kikao cha ndani jijini Dar es Salaam na wajumbe 170 na kuhojiwa.

Julai 15, mwaka huu, Katibu Mkuu Mashinji, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na Mbunge wa Viti Maalum, Zibeda Sakuru, walikamatwa na Polisi wilayani Nyasa, wakati wakiwa kwenye kikao cha ndani.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment