Kesi inayomkabili Mbunge wa Kawe, Halima Mdee anayedaiwa kutumia lugha ya matusi dhidi ya Rais John Magufuli itaanza kusikilizwa Novemba 8 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Usikilizaji utaanza baada ya Wakili wa Serikali, Janeth Magoho kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa kutokana na upelelezi kukamilika.
Mdee anadaiwa kutenda kosa hilo Julai 3 katika ofisi za makao makuu ya Chadema, mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni. Anadaiwa kumtusi Rais akisema, “Anaongea hovyo hovyo, anatakiwa afungwe breki.”
Kauli hiyo inaelezwa ingeweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Baada ya kusomewa maelezo ya awali, Mdee alikubali yanayohusu jina lake, anaishi Makongo, ni mbunge na siku ya tukio, Julai 3 alikuwa eneo la ofisi ya Chadema iliyopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni.
Mdee amekana kutoa lugha ya matusi dhidi ya Rais, bali alikubali Julai 4 alikamatwa akiwa Kibangu wilayani Kinondoni na kupelekwa polisi kwa mahojiano.
Mbunge huyo amekana maelezo kuwa wakati akihojiwa alikubali kutoa lugha ya matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Mdee pia amekubali kuwa alifikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi inayomkabili.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, Novemba 8 upande wa mashtaka utaanza kuwasilisha ushahidi.
Mdee alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Julai 10 na anawakilishwa na mawakili Peter Kibatala, Nashon Nkungu, Jeremiah Mtobesya, Faraja Mangula, Omary Msemo na Hekima Mwasipu.
0 comments :
Post a Comment