Majambazi hao, baada ya kuvamia nyumba ya Meja Makala (44) iliyoko Tuangoma jijini Dar es Salaam, walivunja mlango kwa milipuko kwa nia ya kutaka kuiba lakini walizidiwa maarifa na polisi waliowarushia risasi na wao kujibu mapigo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema majambazi hao walivamia makazi hayo usiku wa kuamkia jana wakiwa na milipuko waliyoitumia kubomolea geti.
“Askari waliwahi eneo la tukio na majambazi hao walifyatua milipuko hali iliyosababisha askari kujibu mashambulizi. Kundi hilo lilitawanyika na kuendelea kufyatua milipuko na katika mashambulizi hayo, majambazi wanne walijeruhiwa kwa risasi sehemu mbalimbali za miili na walifikishwa Hospitali ya Rufani ya Temeke ambako wote walifariki dunia wakipatiwa matibabu,” alisema.
Mambosasa alisema katika eneo la tukio polisi, walikuta nyaya mbili za shaba, betri moja kwa ajili ya kulipua milipuko na mapanga matano.
Pamoja na uvamizi huo, Kamanda Mambosasa alisema Meja huyo wa JWTZ na familia yake wako salama na kwamba juhudi za kuwatafuta majambazi wengine waliokimbia zinaendelea.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa alisema wanawashikilia watu 12 ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo vya kubadilisha vipuli vya pikipiki kutoka kwenye pikipiki moja na kuzifunga kwenye pikipiki nyingine kwa lengo la kubadilisha mwonekano.
Alisema watu hao walikamatwa baada ya kumpiga risasi mguuni mwanafunzi Andrew John (20) na kuporwa pikipiki aliyokuwa anaiendesha Juni, mwaka huu.
“Msako uliendelea kufanyika mpaka tulipowakamata watu hawa 12 eneo la Buguruni Malapa. Askari waliwakuta wakiwa wanafanya kazi ya kubadilisha vipuri vya pikipiki moja kwenda nyingine ili kubadili mwonekano. Tunaendelea kufanya uchunguzi wetu,” alisema.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Hassan Bakari, Daud Augusto na Tido Daudi ambao walikutwa na pikipiki