Serikali inatarajia kutoa ajira kwa wafanyakazi 400 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kipindi kifupi kijacho ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika mamlaka hiyo, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi na makusanyo ya kodi.
Ahadi hiyo imetolewa Mjini Shinyanga na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utendaji wa mamlaka hayo mkoani humo.
Dkt. Kijaji amesema, taratibu zote zimekamilika na wakati wowote nafasi za ajira zitatangazwa na kwamba nafasi hizo zimelenga kuiwezesha TRA kuwafikia watu wengi zaidi na kuongeza wigo wa makusanyo ya kodi.
“Tunatambua changamoto ya uchache wa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ndio maana tumeamua kuajiri wafanyakazi hao 400 ambao ni wengi kuliko kada nyingine ili tuweze kuimarisha utendajikazi wa mamlaka na hivyo kuongeza makusanyo ya kodi zinazotakiwa kwa shughuli za maendeleo nchini” alisema Dkt. Kijaji.Facebook