Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wameuomba uongozi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kuifanyia usafi wa kutosha hospitali hiyo ili ilingane na hadhi yake tofauti na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya vitanda wanavyolalia wagonjwa vinadaiwa kuwa na wadudu aina ya kunguni.
Wakizunguumza na Azam News kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga wenye wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo ya rufaa wameelezea masikitiko yao ya hali ya uchafu kwenye vitanda vya wagonjwa huku vingine vikiwa havina shuka na kusababisha kuwepo kwa wadudu aina ya kunguni.
Dkt. Maguja Daniel ni Kaimu Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambaye amekanusha madai ya kuwepo kwa uchafu na kueleza kuwa kitengo cha usafi hospitalini hapo kinatimiza wajibu wake huku akidai kama kuna kunguni wameonekana huenda waliingia kwa bahati mbaya kutokana na mazingira ya wagonjwa wanaopokelewa na kulazwa hospitalini hapo.
Malalamiko hayo ya wananchi yanaacha maswali mengi kwa kitengo cha afya cha hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga ambacho kazi yake kubwa mbali ya kufanya upulizaji wa dawa za kuua wadudu na kutunza usafi wa mazingira, majengo na miundombinu mbalimbali ya hospitali hiyo.
chanzo;Azam TV
0 comments :
Post a Comment