Mwaka 2005, aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Aden Rage, alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kukutwa na hatia ya kuhusika na wizi wa fedha na mali za kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania (Fat).
Kesi ya msingi ilikuwa kwamba mwaka 1999 Rage akiwa Katibu Mkuu wa Fat, alihusika na wizi wa fedha Sh3,000,000 na mipira 50 mali ya Fat. Kwa makosa hayo alihukumiwa miaka mitatu jela lakini mwishoni mwa mwaka 2005, Rage aliachiwa huru kwa msamaha wa Rais.
Hata baada ya kuachiwa huru, Rage aliendelea na kesi yake ya rufaa ambayo aliifungua kabla ya kupewa msamaha na Rais. Machi 2008, Rage alishinda kesi baada ya majaji watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Damian Lubuva, John Mrosso na Salim Mbarouk kuona hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.
Wanasheria na mahakama kwa jumla, kuna kitu kinaitwa “legal citation”, kwa maana ya mfumo wa kisheria kupitia na kufanya marejeo ya kesi za nyuma na uamuzi wake ili kujenga nguvu ya hukumu katika kesi ambayo inakuwa na sura yenye kufanana.
Nimekumbusha kesi ya Rage kama legal citation ili kujenga hoja katika kile ambacho hivi sasa kinabeba tafsiri ya kuwavua hatia ya kubaka na kulawiti watoto 10, mwamuziki mkongwe nchini, Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’.
Desemba 9, mwaka huu katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, Rais John Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa zaidi ya 1,800 vilevile aliwasamehe 61 waliokuwa wanasubiri kunyongwa na kwa kipekee alisema anawasamehe Babu Seya na Papii Kocha.
Baada ya kuachiwa, kumekuwa na kundi kubwa la watu ambao wanashangilia. Wanafurahi utadhani Babu Seya na Papii Kocha wamefutiwa hatia. Vema kuwakumbusha kwamba msamaha wa Rais haufuti hatia ya mfungwa, isipokuwa Mahakama ndiyo hufanya hivyo.
Rage hata baada ya kuachiwa huru, aliendelea kupambana kisheria Mahakama Kuu mpaka majaji walipomfutia hatia. Ni baada ya kufutiwa na hatia ndiyo maana Rage aliweza kugombea ubunge jimbo la Tabora Mjini na kushinda. Hakuishia hapo alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Klabu ya Simba.
Hivyo basi, watu wasikosee kumuona Babu Seya na mwanaye Papii Kocha kuwa wamesamehewa hatia waliyokutwa nayo, bali itambulike kwamba wamesamehewa adhabu ya kifungo cha maisha jela na sasa wapo uraiani kwa huruma ya Rais Magufuli.
Umuhimu wa kukumbusha
Tangu Babu Seya na wanaye watatu, akiwemo Nguza Mbangu ‘Nguza Machine) na Francis Nguza walipokamatwa kwa mara ya kwanza mwaka 2003 na kutuhumiwa kuhusika na vitendo vya ubakaji na ulawiti wa watoto 10 wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza, Dar es Salaam, mengi yalianza kuzungumzwa.
Badala ya watu wakumbwe na mshituko, vilevile maumivu juu ya taarifa za watoto wadogo kuharibiwa, wengi waliamini uvumi wa mitaani kuwa Babu Seya na wanaye, walitengenezewa kesi na kigogo au vigogo wa Serikali ili kumkomoa mwanamuziki huyo na familia yake.
Tunaishi kwenye nchi moja, kila ambacho kilisemwa kimezunguka na tumekisikia. Ni kwa sababu hiyo hata muda wote Babu Seya na wanaye wakiwa jela, iliendelea kuvuma kwamba wamefungwa kwa uonevu. Ni kwa mantiki hiyohiyo, wengi wameshangilia kutokana na mkumbo.
Wengi ambao wanaamini, wanashupaa kujenga hoja na kusambaza uvumi kuwa Babu Seya alionewa na wanaye, hawakufuatilia msingi wa kesi, wala hawakuwahi kusoma hukumu iliyowatia hatiani kuanzia Mahakama ya Kisutu, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa mpaka Mahakama ya Afrika kuhusu Binadamu na Haki za Watu (ACHPR).
Hawajui nguvu ya mashitaka na uwepo wa watoto ambao walipimwa na kuthibitishwa kweli waliharibiwa kwa kubakwa na kulawitiwa. Hawatambui kama wapo waliokutwa na maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STD) aina ya kaswende. Hawajasoma simulizi za watoto hao na namna jina la Babu Seya lilivyoanza.
Hapo ndipo unaipata taswira ya Tanzania na Watanzania. Wanaweza kuhukumu kwa kusikia au kutetea kwa sababu wameambiwa na mtu ambaye naye amesikia. Mtu kapewa umbea kwamba Babu Seya na familia yake wanakomolewa, kwa hiyo anasambaza na wanaosambaziwa pia wanaeneza, kutahamaki uvumi unaenea kuliko ukweli.
Mzazi mwenye watoto wake anaowapenda, hafikirii uchungu walionao wazazi ambao watoto wao wameharibiwa au maumivu na athari ya ukuaji ambayo watoto husika watakuwa wameipata kutokana na vitendo walivyofanyiwa, anaketi kibarazani na kusogoa kwamba Babu Seya anasingiziwa.
Fikiria angekuwa mwanao
Kama wewe ni mwanamke, jiweke katika nafasi ya mama wa mtoto ambaye alikuwa anaishi kwa mjomba wake, yaani kaka yako. Halafu wifi yako anagundua kwamba mwanao akikaa anatoa harufu. Anamwambia mtoto akaoge lakini bado harufu haiishi. Anapofuatilia anagundua mtoto kaharibiwa na zaidi ameambukizwa kaswende.
Jiweke nafasi ya baba wa yule mtoto ambaye anaishi kwa mjomba wake. Unapewa taarifa kuwa binti yako mwenye umri wa miaka sita ni mwathirika wa vitendo vya kubakwa na kuingiliwa kinyume na maumbile. Unajulishwa kwamba waliomfanyia hivyo binti yako walimrubuni kwa Sh200 na pipi.
Ni uhakika kama wewe ni mzazi mwenye uchungu na mwanao na unawajibika vizuri katika malezi, mtoto wako angekueleza aliyotendewa mithili ya watoto wa tukio la Babu Seya walivyosimulia mahakamani, kisha vipimo vithibitishe kweli walifanyiwa ukatili, pengine ungeapa kutowasamehe wahusika maisha yako yote.
Ufafanuzi huo unalenga kukumbusha kuwa kadiri maneno na sauti za watu zinavyopazwa kuwa Babu Seya na wanaye walionewa, upande wa pili ni maumivu makali kwa wazazi na familia za watoto waliothibitika kutendewa unyama wa kijinsia. Zaidi ni wale watoto ambao kwa sasa ni watu wazima.
Kwa tafsiri pana zaidi ni kuwa maneno kuwa Babu Seya na wanaye walionewa, yanawawakilisha Watanzania kuhusu uwezo wa kujiuliza na kupata majibu. Kweli kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa mara mbi hadi Mahakama ya Afrika, wanaonewa tu?
Tuheshimu Mahakama
Oktoba 8, 2003 ndiyo sakata lilianza. Shahidi wa kwanza kwenye kesi hiyo anasimulia kuwa aligundua mtoto wa wifi yake (shahidi wa pili) anatoa harufu na alipomchunguza aligundua anatoka damu sehemu za siri na alikuwa na mabaki ya kinyesi sehemu ya haja kubwa. Mtoto huyo alikuwa anasoma darasa la kwanza.
Oktoba 9, 2003 anazungumza na mtoto, hasa baada ya kupata taarifa kutoka kwa dada wa kazi, aliyesema aliwahi kumuona mtoto ana Sh200 aliyosema alipewa na Babu Seya. Mtoto baada ya kuahidiwa asingeadhibiwa, alieleza namna alivyorubuniwa na Babu Seya pamoja na vitendo vyote alivyofanyiwa.
Mtoto akasema hakuwa peke yake, alikuwa na watoto wenzake, akawataja majina. Mama huyo (shahidi namba moja), siku hiyohiyo alikwenda kufungua jalada Kituo cha Polisi Urafiki na kupewa fomu ya polisi namba 3 (PF3) kwa ajili ya matibabu. Baada ya hapo alimpeleka Hospitali ya Mwananyamala na kukutwa kweli ameathiriwa na alikuwa ameambukizwa kaswende.
Oktoba 10, 2003, shahidi namba moja alikwenda Shule ya Msingi Mashujaa na kuzungumza na uongozi wa shule na kuuomba utafute ukweli kuhusiana na watoto ambao walitajwa majina na mtoto shahidi namba mbili, kwamba walikuwa wakienda wote kwa Babu Seya.
Baada ya hapo ndipo watoto husika walipoanza kusimulia kila kitu. Oktoba 12, 2003 Babu Seya na wanaye watatu walikamatwa wakiwa kwenye nyumba ambayo ilitajwa na watoto, namba 607 Sinza B na kushikiliwa kituo cha polisi Urafiki kabla ya kuhamishiwa Magomeni.
Oktoba 16, 2003, Babu Seya na wanaye watatu, Papii Kocha, Mbangu na Francis pamoja na mshitakiwa wa tano ambaye alitajwa kuwa mwalimu, walifikishwa Mahakama ya Kisutu na kusomewa mashitaka 10 ya ubakaji na 11 ya ulawiti. Juni 25, 2004, walihukumiwa kifungo cha maisha jela, huku mwalimu (mtuhumiwa wa tano) akiachiwa huru.
Sababu ya kuibuka kwa jina la Babu Seya ni kwamba wakati sakata hilo linashika kasi, wimbo Seya ulikuwa maarufu mno. Seya ni wimbo wa Nguza Vicking lakini mwaka 2003 uliimbwa kwa mara ya pili na Papii Kocha kwa kushirikiana na Nguza mwenyewe.
Watoto ambao walifanyiwa vitendo vya kubakwa na kulawitiwa ndiyo sababu ya kuwepo jina hilo la Babu Seya, kwani ndivyo ambavyo walikuwa wakimwita. Kabla ya hapo, jina hilo halikuwa likitambulika, zaidi Seya lilifahamika lilikuwa jina la wimbo wa Papii Kocha na baba yake, Nguza.
Baada ya hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu, Babu Seya na wanaye walikata rufaa Mahakama Kuu ambako Jaji Thomas Mihayo alitupilia mbali rufaa hiyo. Nimesoma hukumu ya Jaji Mihayo, kwa hakika inajibu kila hoja ya rufaa kwa misingi ya kisheria na vielelezo bila kuacha shaka.
Walipotoka Mahakama Kuu walikata rufaa Mahakama ya Rufaa, ambako Mbangu na Francis waliachiwa huru. Babu Seya na Papii Kocha waliendelea kukutwa na hatia ya makosa manne ya kubaka. Walikata rufaa kwa mara nyingine kuomba shauri lao lipitiwe upya lakini Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa yao.
Mwaka 2015, Babu Seya na Papii Kocha walifungua shauri namba 006/2015 kwenye Mahakama ya Afrika kuhusu Binadamu na Haki za Watu (ACHPR) na hukumu ilitoka na kuendelea kuwabakiza Babu Seya na Papii Kocha kwenye kifungo cha maisha jela.
Mapitio hayo yanaonyesha kuwa kwa sehemu kubwa haki inaonekana kutendeka, maana walipewa haki zote za kukata rufaa na kushindwa. Kisutu mpaka Mahakama ya Afrika, waliendelea kuwa na hatia, hivyo wakati watu wakishangilia Babu Seya na Papii Kocha kuachiwa, watambue kuwa hawajafutiwa hatia, bali wamesamehewa adhabu.
0 comments :
Post a Comment