Mamia ya waombolezaji wakiwemo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Viongozi wa serikali na vyama vya siasa na wananchi leo Ijumaa Disemba 15,2017 wamejitokeza kumzika askari wa JWTZ Private Saleh Said Mahembano (30) katika makaburi ya nyumbani kwao katika mtaa wa Isaka Station halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Private Mahembano ni miongoni wa askari 14 waliouawa nchini Kongo Disemba 8,2017 wakati wakitekeleza jukumu la ulinzi na amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ambapo walivamiwa na waasi waliojulikana kuwa ni ADF na kusababisha mauaji kwa wanajeshi 14 na wengine 44 kujeruhiwa.
Mazishi ya Private Mahembano aliyezikwa kwa heshima za kijeshi yameongozwa na Kamanda wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kanda ya Shinyanga,Kanali Mussa Kingai.
Akizungumza wakati wa mazishi hayo,Kanali Kingai alisema kifo cha Mahembano ni cha kishujaa kwani aliweza kutoa upinzani kwa adui aliyewashambulia
“Askari hawa waliopoteza maisha ni mashujaa wetu,tunawaenzi sana,inawezekana kwa kitendo walichokifanya historia ya Kongo itabadilika,serikali imetoa maagizo uchunguzi ufanyike kuhusu tukio hili,na kama kuna itabainika kuna mtu alitusaliti hatua zitachukuliwa”, alisema Kanali Kingai.
Kanali Kingai alitumia fursa hiyo kuipa pole familia ya marehemu na wananchi kwa ujumla kufuatia kumpoteza mpendwa wao.
Kwa upande wake,Katibu tawala wilaya ya Kahama,Timoth Ndanya aliyemwakilisha mkuu wa mkoa wa Shinyanga aliiomba familia ya marehemu na wananchi kuwa na subira katika kipindi hiki kigumu.
0 comments :
Post a Comment