Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ameondoka jana kwenda Ubelgiji kwa matibabu zaidi huku akisema atamsubiri kwa hamu Spika wa Bunge, Job Ndugai kwenda kumtembelea huko.
Kadhalika, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema amesisitiza wito wake wa kuwataka wanachama wa upinzani kutokurudi nyuma katika mapambano dhidi ya demokrasia.
Akiagana na wanachama na viongozi wa Chadema waliofika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya kumsindikiza kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Jomo Kenyatta(JKIA) jana, Lissu alisema anaamini kwamba Spika Ndugai ambaye alipanga kumtembelea Nairobi baada ya sikukuu lakini ikashindikana, atatimiza ahadi yake kwa kwenda Ubelgiji.
Akizungumza kwa sauti yenye kusisitiza Lissu alisema “Aliwaambia (Spika Ndugai) Watanzania kwamba angekuja kuniona tarehe tatu au nne (Januari) na leo (jana) tarehe sita naondoka, naenda kumsubiri Ubelgiji.”
Hata hivyo, Spika Ndugai hakupatikana jana kuzungumzia kauli hiyo ya Lissu baada ya simu yake kuita bila kupokewa kila alipopigiwa.
Lissu ambaye alishambuliwa kwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari katika makazi yake mjini Dodoma, Septemba 7 mwaka jana, aliondoka jana saa 2:30 asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) akiambatana na mkewe, Alicia.
Akiwa hospitalini hapo jana saa kumi na moja alfajiri, Lissu ambaye wakati wote alikuwa mwenye furaha na tabasamu, aliagana na kila mmoja aliyefika kumsindikiza, na mara alipoonana na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Rose Kamili aliyempa vazi la kimasai Lissu alisema “Watanikoma… siku ninarudi watanikoma.”
Alirudia kauli hiyo alipoulizwa na mwandishi wetu ni ujumbe gani anawaachia Watanzania na kuongeza, “Nitasimama, nitatembea, nitarudi na mapambano yataendelea sasa chapeni kazi, mimi nitarudi kuendeleza mapambano haya.
“Baada ya miezi minne ya kutibiwa Hospitali ya Nairobi na baada ya hali niliyonayo sasa hivi, naingia hatua ya mwisho ya kwenda kukamilisha kazi ya kuuponya huu mwili na kurudi nyumbani kuendelea na mapambano.”
Hakuacha kutoa shukurani akisema, “Wakenya wameokoa maisha yangu na Wakenya wamenilinda, askari wao wamenilinda saa 24 usiku na mchana katika kipindi chote hicho na kwa sababu hiyo nina shukrani kubwa kwa nchi ya Kenya na serikali yao.
“Nchi ya Kenya kwa sababu madaktari wao na askari wao ndio walionilinda. Nawashukuru pia madaktari wa Dodoma kwa sababu wao ndio waliokuwa wa kwanza kuokoa maisha yangu na nimshukuru kipekee Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya (Dk Mpoki Ulisubisya) kwa sababu mengi yalifanyika chini yake,” aliongeza.
Ndugu, jamaa, marafiki, viongozi na wanachama wa Chadema, walianza kufika hospitalini hapo saa 10 alfajiri ili kumsindikiza Lissu ambaye amepewa na magongo ya kumwezesha kutembea akiwa huko.
Msafara wa kutoka hospitalini kwenda Uwanja wa Ndege wa Kenyatta ulianza saa 11.41 alfajiri ukiwa chini ya ulinzi wa askari zaidi ya watatu wenye silaha waliokuwapo hospitalini hapo na wengine waliongezeka mara baada ya kuwasili uwanjani hapo.
Miongoni mwa waliokuwapo kumsindikiza ni watoto wake pacha, Agustino na Edward (15), kaka yake, Alute Mughwai na mgodo wake, Dk Vincent Mughwai.
Pia, alikuwapo Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji aliyesema gharama za safari hiyo na matibabu zimegharamiwa na Chadema pamoja na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambacho Lissu ni Rais wake.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Alute alisema, “Tunamwomba Mwenyezi Mungu huko atakakokwenda aweze kupata matibabu mazuri, ameondoka vizuri, anazungumza na sisi tumefarijika. Kwa niaba ya familia, nitoe shukrani zetu kwa wananchi wa Tanzania na wale wa Kenya ambao wametuunga mkono mpaka leo (jana) anavyoondoka hapa.”
Mkuu wa Idara ya Uenezi wa Chadema, Ally Hemed ambaye alikuwa akisimamia matibabu ya Lissu tangu alipofikishwa hospitalini hapo alisema “Ni jambo la kumshukuru Mungu. Tulimpokea mwili wake ulikuwa na mashaka mengi, lakini kupitia kwake nimeona miujiza mingi.
“Katika kipindi cha miezi minne, nimejifunza na nimepata darasa katika kupata ujasiri wa kupigania demokrasaia, kuna mafunzo na faraja lakini yote Mwenyezi Mungu amesimamia, tunawashukuru wote hasa Mwenyekiti (Freeman) Mbowe kwa kutuongoza hadi tulipofika.”
Dk Mashinji alisema wana faraja kuona mwanasheria wao mkuu akiwa na afya iliyoimarika na kilichobaki ni viungo tu na Lissu waliyekuwa wanamjua ndiye huyohuyo aliye sasa.
“Tunawashukuru sana madaktari wa Dodoma, bila wao tusingekuwa na Lissu leo, pia madaktari wa Kenya, tunawashukuru sana. Lissu kwa sasa yuko imara, anakwenda kwa mazoezi ya kurudisha viungo vyake salama na kumjenga kisaikolojia.
“Sisi kama chama pia si vibaya kama tunajipongeza kwa kufanya uamuzi sahihi na wa haraka kwa kuhakikisha watu wanaotetea masilahi mapana ya Taifa tunawalinda... tunahitaji kuweka mazingira yatakayotoa ulinzi kwa viongozi wetu,” aliongeza Dk Mashinji.
0 comments :
Post a Comment