Mahakama ya Rufaa imemwondolea Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mamlaka ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa bila hata kulazimika kutoa sababu, baada ya kubatilisha kifungu cha 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, kinachompa mamlaka hayo.
Kifungu hicho kinampa DPP mamlaka ya kuizuia Mahakama au ofisa wa polisi kutoa dhamana kwa mshtakiwa au mtuhumiwa baada ya kuwasilisha hati ya maandishi, kwa maelezo kuwa usalama au masilahi ya Jamhuri yataathirika.
Mahakama hiyo katika hukumu ya rufaa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya mwanaharakati wa haki za binadamu, Jeremia Mtobesya imesema kifungu hicho ni kinyume cha Katiba na ni batili.
Hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watano wa Mahakama ya Rufaa imekubaliana na ya awali iliyotolewa na Mahakama Kuu.
Majaji waliosikiliza na kutoa hukumu ya rufaa hiyo ni Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Kipenka Mussa, Bethuel Mmila, Stellah Mugasha na Jacob Mwambegele.
Hukumu hiyo ilisomwa Ijumaa iliyopita na Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza aliyesema kifungu hicho kwa jinsi kilivyo, Mahakama au ofisa wa Polisi anakuwa hana uchaguzi zaidi ya kumnyima dhamana mshtakiwa au mtuhumiwa.
Alisema kifungu hicho hakikidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa haipaswi kuwa ya maelezo ya jumla na kinaweza kutoa mwanya wa matumizi mabaya ya mamlaka kwa DPP.
Baada ya kufanya rejea ya sheria na uamuzi wa kesi kadhaa za ndani na nje ya nchi, Kahyoza alisema Mahakama imejiridhisha kuwa masharti ya kifungu hicho ni kinyume cha Katiba na hivyo ni batili.
Akizungumzia jana kuhusu hukumu hiyo, Mtobesya alisema Mahakama imeitoa kwa misingi ya kikatiba.
“Katiba ndivyo inavyoelekeza kuwa mtu yeyote ana haki ya kusikilizwa na kila mtu ana haki ya kuwa huru. Sasa iwapo hizo haki zinaweza zikaondolewa, kuna utaratibu ambao unawekwa kisheria,” alisema.
Mtobesya alisema, “Kwenye ngazi zote, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa zimeangalia na kujiridhisha kwamba sawa hizo haki zinaweza kuwa si absolute (kamilifu) lakini je misingi ya kunyimwa hizo haki imefuatwa?”
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikata rufaa akipinga hukumu ya Mahakama Kuu ya Desemba 22,2015 iliyotolewa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Kiongozi, wakati huo, Shaban Lila. Majaji wengine walikuwa Sekieti Kihiyo na Profesa Eudes Ruhangisa. Katika shauri la msingi la madai namba 29 la mwaka 2015, Mtobesya ambaye ni wakili wa kujitegemea alidai kifungu hicho kwa jinsi kilivyo kinamnyima mshtakiwa aliye mahakamani au mtuhumiwa aliye polisi haki ya kusikilizwa.
Katika hoja za maandishi, alidai kila kesi inaangaliwa kwa mazingira yake na kwamba, kitendo cha DPP kuzuia tu dhamana kwa madai kwamba itaathiri masilahi ya umma bila kutoa sababu kinamnyima haki mhusika.
Alidai maelezo hayo tu ya kuathiri masilahi ya umma hayatoshi bali anapaswa kwenda mbali zaidi na kutoa sababu na kisha mshtakiwa au mtuhumiwa naye apewe nafasi ya kusikilizwa ndipo Mahakama ipime na kutoa uamuzi kwa sababu hizo.
Mahakama Kuu katika hukumu yake ilikubaliana na hoja za Mtobesya, ikisema kifungu hicho kinamnyima mtu haki ya kusikilizwa na ni kinyume cha Ibara ya 13 (6) ya Katiba ya nchi.
Mahakama ilisema kifungu hicho kinaenda kinyume cha misingi ya kidemokrasia.
Hukumu hiyo katika kesi ya jinai, DPP na mshtakiwa wote wanakuwa na haki sawa lakini kifungu hicho kinaupa upande mmoja mamlaka zaidi na kuufanya mwingine kuwa dhaifu, hivyo kutokuwa na usawa.
Mahakama Kuu ilisema kifungu hicho kinaondoa mamlaka ya Mahakama kuwasikiliza wadaiwa.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakukubaliana na uamuzi huo, hivyo alikata rufaa Mahakama ya Rufaa akiwasilisha hoja tano za kuipinga. Wakati wa usikilizwaji aliondoa hoja tatu zikabaki mbili.
Pamoja na mambo mengine, AG aliipinga hukumu hiyo akidai kifungu hicho kiko sawa kwa kuwa kuna ibara za Katiba ambazo zinakifanya kiwe hivyo kilivyo, sawa na ibara ya 30 (2) (a) ya Katiba.
Mtobesya kupitia kwa wakili wake Mpale Mpoki alipinga hoja zilizotolewa na AG kupitia Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timon akidai kifungu hicho kwa namna kilivyo hakimpi fursa mshtakiwa kusikilizwa kabla ya kuzuiwa dhamana kwa hati ya DPP.
Wakili Mpoki alidai kifungu hicho kinakiuka ibara ya 13 (6) ya Katiba ya nchi, huku akiungwa mkono na Profesa Gamaliel Mgongo Fimbo aliyealikwa na Mahakama kutoa maoni ya kitaalamu.
Profesa Mgongo Fimbo pamoja na mambo mengine alisema kifungu kinachomzuia mshtakiwa kusikilizwa maombi yake ya dhamana au kupinga hati ya DPP, hakiweki usawa wa usikilizwaji, hivyo kinakiuka ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba.
0 comments :
Post a Comment