Mfanya biashara James Rugemalila anayekabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha na uhujumu uchumi leo Ijumaa Februari 2, 2018 ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa hajawahi kutibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Rugemalira ametoa madai hayo baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa washtakiwa katika kesi hiyo wanatibiwa Muhimbili.
Rugemalira na mwenzake Habinder Sethi ambaye ni Mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha Serikali hasara.
" Mheshimiwa hakimu sijapelekwa Muhimbili kutibiwa na wala sijawahi kutibiwa, bado nina uvimbe ambao ninahisi ni saratani" amedai Rugemalira.
Amesema anaomba apatiwe kibali cha kwenda kutibiwa India ambako ndipo alipotibiwa kipindi cha nyuma baada ya kugundulika kuwa na saratani.
"Daktari wangu na hospitali ninayotibiwa ipo India, hivyo upelelelezi unavyochelewa na hili dude (uvimbe) lilivyovimba ndio nazidi kuchanganyikiwa," amesema Rugemalira,
"Nataka kuweka kumbukumbu sawa, daktari wangu Fred kutoka hospitali ya Sanitas nilitaka aje aonyeshe vipimo vyake kama kweli sina saratani, lakini kwa bahati mbaya amefiwa na leo hayupo mahakamani."
Mshtakiwa huyo amedai hata muda wa kwenda kufanyiwa uchunguzi umeshapita kwani alitakiwa kwenda India kati ya Julai na Septemba mwaka 2017, lakini alishindwa kwa kuwa yupo rumande.
" Mheshimiwa huu uvimbe wangu ni saratani tu, kwa sababu nimeshapitia katika hali kama hii kwa miaka 10, ndio maana naomba kwenda kutibiwa India kwa sababu kule kuna vifaa vya kisasa"amedai.
Kutokana na madai hayo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Huruma Shahidi amesema madaktari wa MNH ndio wenye kuthibitisha mshtakiwa akatibiwe wapi.
Awali, Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amedai mahakamani hapo kuwa Serikali inajitahidi kuchukua hatua stahiki katika kuwapatia matibabu washtakiwa hao ikiwemo kuwapelekea Muhimbili.
Hakimu Shahidi ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 16, 2018 itakapotajwa na washtakiwa hao kurudishwa rumande.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kuisababisha serikali hasara ya dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh 309,461,300,158.27
0 comments :
Post a Comment