Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo Mhe. Zitto Kabwe amefunguka na kusema kuwa deni la taifa limeweza kuongezeka kwa asilimia 168% ndani ya muda mfupi toka Serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani.
Zitto Kabwe amesema hayo Januari 1, 2018 wakati akichangia Bungeni na kudai kuwa kwa mujibu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad ndani ya kipindi kifupi deni la taifa limeongezeka.
"Ukitizama aliyosema CAG kuhusu deni la taifa inaonyesha kwamba ndani ya kipindi kifupi sana deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 168% lakini baya zaidi deni ambalo linatokana na masharti ya biashara limeongezeka kwa asilimia 17 ndani ya mwaka mmoja, madeni yanayotokana na masharti ya biashara gharama zake ni kubwa sana na inawezekana uwezo wetu wa kuyalipa ukawa na matatizo makubwa sana. Ndani ya taarifa hii ya CAG inaonesha kwamba taarifa ambayo Serikali ilitoa kuhusu deni la Taifa, deni la jumla ya tilioni 3.2 halikuwepo kwenye taarifa ya deni la Taifa, tulitarajia leo tungepata maelezo kwanini tilioni 3.2 hazikuhusisha katika taarifa ya pamoja ya deni la Taifa" alisema Zitto Kabwe
Mbali na hilo Zitto Kabwe alimjia juu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango na Naibu wake kwa kitendo cha kuwadanganya wananchii juu ya ujenzi wa reli mpya wa kisasa Standard Gauge kwa kusema inajengwa kwa fedha za ndani ili hali Serikali inakopa fedha ili kujenga reli hiyo.
"Serikali imekamilisha majadiliano na taasisi za kifedha kwa lengo la kukopa kiasi cha dollar za Marekani Bilioni 1.5 kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha 'standard gauge' kutoka Morogoro hadi Makutopora Serikali inakamilisha utaratibu wa kusaini mkataba. Waziri Mpango ruhusa uliyopewa na Bunge ni kukopa dollar za Marekani Milioni 700 ni wapi ulipata ruhusa ya kwenda kujadiliana kukopa ziada ya 1.5 Bilioni ?
Zitto Kabwe aliendelea kuhoji
"Wabunge wote humu ndani ni mashahidi kila siku tunaambiwa, tunajenga reli ya Standa gauge kwa fedha zetu za ndani lakini leo Serikali inasema tunakopa, Kwanini tunawalaghai wananchi? Kwanini hatuwaelezi wananchi ukweli kwamba hatuna uwezo wa kujenga kwa fedha za ndani lakini tunakopa, kuna ubaya gani maanake kukupa si dhambi, kwanini tunamuacha Rais anasema tunajenga reli kwa fedha zetu za ndani halafu tunakuja Bungeni taarifa za Serikali zinasema kwamba tunakopa mnamuaibisha Rais" alisisitiza Zitto Kabwe
0 comments :
Post a Comment