Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu ameitaka Serikali kulieleza Bunge ni lini itajenga reli kipande cha Makotopora– Kigoma hadi Mpanda na baadaye kipande cha Isaka hadi Kigali.
Kanyasu ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Juni 1, 2018 wakati akiuliza swali la nyongeza huku akitaja pia ujenzi wa reli ya kisasa katika mikoa ya Geita na Kagera.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye amesema kwa sasa Serikali imeshakamilisha taratibu za ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam- Morogoro hadi Makotopora (Dodoma).
“Kuhusu ujenzi wa kipande cha Geita – Kagera hadi Uganda, mchakato bado unaendelea na mara fedha zitakapopatikana mbunge atajulishwa,” amesema Nditiye.
Amesema Serikali inatambua kila nchi ina wajibu wa kutekeleza mradi wa kujenga reli hiyo katika sehemu yake, kwamba ni wajibu wa kila nchi kukamilisha mradi huo ili kuchochea maendeleo yanayotokana na ujenzi wa reli hiyo.
Kuhusu kipande cha reli ya Isaka kupitia Kabanga hadi Rusumo na Kigali nchini Rwanda, amesema Serikali inakamilisha maandalizi ya ujenzi wake na mkataba na usanifu na matayarisho ya zabuni umesainiwa na kazi itaanza Juni 2018
0 comments :
Post a Comment