Sekta ya madini imekua kwa asilimia 17.5 ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya mwaka 2016 ambapo ongezeko hilo limetokana na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini, kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini pamoja na usafirishaji wa madini nje ya nchi.
Waziri wa Madini,Angellah Kairuki amesema hayo jana,Mei 31, 2018 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
“Ukuaji wa sekta ya madini pia kumetokana na kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 na kanuni zake,” alisema Angellah Kairuki.
Aidha alisema, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika mwaka 2017 mchango huo ulifikia asilimoa 4.8. Kwa upande wa thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi, mauzo yalifikia Dola za Marekani 1,810,697,000 mwaka 2017.
“Ni matarajio yetu kuwa thamani ya mauzo inaendelea kuongezeka tena baada ya kukamilisha mageuzi makubwa ambayo tuliyaanzisha ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani madini ndani ya chini,” alisema Mhe. Kairuki.
Waziri Kairuki alizitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 na Wizara ya Madini na Taasisi zake kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.
Alizitaja kazi nyingine kuwa ni kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa, kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya Sekta ya Madini, kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini, kuelimisha Umma na kuboresha mawasiliano kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini.
Wizara ya Madini imeomba kuidhinishiwa na Bunge jumla ya shilingi 58,908,481,992 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2018/2019
0 comments :
Post a Comment