Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Aiagiza Tamisemi Kutenga Maeneo Maalumu Ya Wamachinga

Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogowadogo (Wamachinga) ili waweze kufanya biashara zao bia bughdha yoyote.

Maagizo hayo yametolewa Jijini Dodoma kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Shirika la Umoja wa Machinga (SHIUMA) na kuongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wafanyabiashara hao wanashiriki kukuza biashara zao na pato la Taifa.

Dkt. Kijaji alisema kuwa wamachinga na wajasiriamali wengine wanapokosa maeneo maalumu ya kufanyia biashara zao inakuwa vigumukupata mikopo kutokana na kutotambuliwa, hivyo Sekta za Fedha zikiwemo Benki kuwa na wasiwasi na urejeshwaji wa Fedha hizo hivyo hatua ya kuwatambua itasaidia kutatua changamoto hiyo.

 “Tanzania inatarajia kuwa na uchumi wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025 na wafanyabiashara wakiwemo wamachinga ndio watakaowezesha kufikia lengo hilo kwa kulipa kodi, hivyo Serikali inachokifanya inaweka mazingira mazuri ya kazi kwa wafanya biashara”, alisema Dkt. Kijaji.

Alisema kuwa baada ya maombi ya muda mrefu ya Wamachinga kutaka kutambuliwa, Serikali katika Sheria ya fedha ya mwaka 2017/18 imeanza kutekeleza maombi hayo kwa kuhakikisha wanatambuliwa na kupewa vitambulisho vya Taifa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ili kurahisha utendaji kazi wao hasa na Sekta ya Fedha kwa kupata mikopo.

Dkt. Kijaji ameipongeza Benki ya NMB ambayo imeendelea kukutana na kuwafadhili wafanyabiashara wadogo ukiwemo Mkutano huo wa SHIUMA kwa kuwa wanatekeleza kwa vitendo azma ya Sekta ya Fedha kuwafikia wananchi wa hali ya chini

Aidha, alirejea pongezi zake kwa baadhi ya benki hapa nchini ikiwemo NMB, CRDB na ABC kwa uamuzi wao wa kushusha riba za mikopo yao na kueleza matumaini yake kwamba wamachinga na wajasiriamali wengine watachangamkia fursa za mikopo hiyo.

Alisema Desemba, 2017 Serikali ilizindua Sera ya huduma ndogo za Fedha itakayowezesha kutambua Taasisi zote ndogo za Fedha zinazokopesha wananchi ili ziweze kuzingatia kanuni za utawala bora zitakazosaidia wafanyabiashara wadogo kukopa kwa kufuata sheria ili kuondoa kudhurumiwa.

Aidha amewapongeza wanachama wa SHIUMA kwa kuanzisha umoja wao utakaosaidia Serikali kupeleka huduma kwa urahisi na kwa usahihi kwa manufaa ya wafanyabiashara na Taifa kwa ujumla na akaahidi kuwa Serikali ipo pamoja nao kwa kuwa ni Serikali inayojali wanyonge.

Akizungumza kwaniaba ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Nchini-IGP Simon Sirro, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Kipolisi ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi-Lazaro Mambosasa, amewapiga marufuku watu wote wanaopora mali za wamachinga nchi nzima.

Alisema kuwa Jeshi lake litawachukulia hatua kali wale wote watakaojihusisha kwa namna moja au nyingine kunyang’anya ama kutaifisha bidhaa za wafanyabiashara wadogowadogo popote pale kwa kuwa vitendo hivyo havikubaliki.

 “Watu wote waliokuwa wanajipatia mali za wamachinga kwa kuwanyanganya bila kupeleka kwenye Mamlaka husika na badala yake wanauza na kutumia huoni unyang’anyi na atakayefanya hivyo atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Alisema Umoja huo wa wamachinga usikubali kushawishiwa kwa nia ovu na watu na baaada ya kujinufaisha binafsi wanawaacha wafanyabiashara hao bila chochote.

Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Machinga Bw. Ernest Masanja alisema kuwa Wanaunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa imeonesha nia ya kuwajali wanyonge hasa wamachinga.

Bw. Masanja alisema katika Mkutano huo wameazimia kushirikiana na TRA wakati wa kutoa semina kuhusu namana ya kulipa kodi na pia wanachama wa vikundi vyote vya wamachinga vilivyo sajiliwa wapewe vitambulisho vya Taifa ili wasajiliwe na Mamlaka hiyo.

Naye Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Dodoma Bw. Peter Kundy alieleza kuwa mpaka sasa kwa Wilaya ya Dodoma Mjini, zoezi la Uhakiki na uandikishaji kwa ajili ya vitambulisho vya Taifa imefanyika kwa kata 41 na zimesalia 6 pekee na zoezi lililobaki ni kutoa pingamizi kwa wasio stahili ili ifikapo Desemba zoezi hilo la utoaji vitambulisho litakuwa limekamilika.

Alisema  zaidi ya watumishi mia tano kutoka Idara ya Uhamiaji wamepelekwa nchi nzima ili kuharakisha zoezi la upatikanaji wa vitambulisho hivyo ili kusaidia katika upatikanaji wa mikopo katika sekta za fedha, elimu, afya na hata hati za kusafiria nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za uchumi.

Shirika la Umoja wa Wamachinga (SHIUMA), limeanzishwa hivi karibuni likiwa na lengo la kuwaunganisha wafanyabishara wadogo wadogo nchini kote
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment