Rais
wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) Dk Ali Mohamed Shein kesho atazindua
Baraza la Wawakilishi la tisa huku akitarajia kutoa mwelekeo wa Serikali
yake mpya iliyopatikana baada ya Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20
uliotawaliwa na mgawanyiko wa kisiasa.
Tofauti
na hotuba yake ya ufunguzi ya Novemba 2010, Dk Shein atahutubia baraza
hilo likiwa na wabunge wa chama kimoja cha CCM baada ya vyama vya
upinzani vilivyotangaza kushiriki uchaguzi wa marudio kushindwa kupata
viti vya uwakilishi.
Pia,
atahutubia akiwa bado hajamteua Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na
matokeo ya uchaguzi huo kutofanikisha kupatikana chama cha upinzani
chenye kura zisizopungua asilimia 10 za kufanikisha kuundwa kwa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Chama
kikuu cha upinzani cha CUF na vingine tisa vilisusia kushiriki uchaguzi
huo baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kufutwa na
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha
kutokana na sababu za uvunjifu wa taratibu na sheria za uchaguzi.
Hata
hivyo, majina ya wagombea wa vyama hivyo yalijumuishwa kwenye karatasi
za kura na kusababisha kuvuna kura kidogo ambazo hazikitosha kutoa
Makamu wa Kwanza wa Rais na Wawakilishi ambao miongoni mwao huteuliwa
kuwa mawaziri wa SMZ.
Tayari
Dk Shein alishaeleza kiufupi baada ya kuapishwa majuma mawili
yaliyopita kuwa Serikali yake itakuwa shirikishi kwa kujumuisha upinzani
na haitabagua katika utoaji wa huduma za jamii katika kuwaletea
wananchi maendeleo.
Jambo
kubwa ambalo Wazanzibari wengi wanasubiri kulisikia kutoka kwa kiongozi
huyo ni iwapo ataeleza kinagaubaga namna atakavyokabiliana na mtanzuko
wa kikatiba wakati wa uundaji wa SUK.



0 comments :
Post a Comment