Mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa makampuni, Ali Mufuruki
(Kushoto) akiangalia kitabu cha Azimio la Tabora alilokabidhiwa na
kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe (wa pili kushoto) baada
ya kumalizika kwa mdahalo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Wengine
ni Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa
Ibrahim Lipumba
.
Dar es Salaam. Viongozi wa vyama vya siasa vya
CUF, NCCR-Mageuzi, NLD na ACT-Wazalendo wameitupia lawama Serikali kwa
kushindwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG).
Wakizungumza kwenye mdahalo wa Uchaguzi Mkuu mwaka
2015 kuhusu masuala ya Sera juzi jijini hapa, viongozi hao Mwenyekiti
wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, Mwenyetiki wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi na Kiongozi wa
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe walisema kuwepo kwa mfumo mbovu serikalini na
kukithiri kwa rushwa ndiyo chanjo cha kupuuzwa kwa ripoti za CAG.
Kwa mujibu wa ripoti ya ukaguzi maalumu wa miaka
mitano ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, imeeleza
bayana kumekuwepo na ufisadi wa takribani Sh600 bilioni zilizochotwa
katika matumizi mbalimbali ambayo hayana maelezo ya kutosha.
Ripoti hiyo maalumu inaonyesha kuwa uovu huo
umekuwa ukiwezekana kutokana na mapendekezo ya CAG ya kuziba mianya ya
upotevu wa fedha, kutofanyiwa kazi.
Akifungua mdahalo huo, Mwenyekiti wa Umoja wa
Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini (CEOrt), Ali Mufuruki
alisema kuwa awali mdahalo huo uliwalenga wagombea kiti cha urais,
lakini kwa kuwa wengi walishindwa kushiriki kwa sababu mbalimbali, sasa
utaitwa mdahalo wa uchaguzi mkuu kuhusu sera.
“Ni matumaini yetu kuwa kushiriki mdahalo kwa njia
hii kutaleta ujumbe ule ule tuliokuwa tumeukusudia kutoka kwa
waliotangaza nia, ambapo masuala ya uchumi, utawala bora na utawala wa
sheria yatakuwa msingi wa mazungumzo,” alisema Mufuruki.
Akijibu swali kuhusu kupuuzwa kwa ripoti za CAG,
Zitto alisema kuwa ili kazi ya CAG iwe bora ni vyema idara za Polisi,
Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (Takukuru) zishirikishwe katika kuchukua hatua zinazostahili.
“Kuijadili ripoti ya CAG pekee yake haitoshi.
Tatizo hili linatokana na kuwepo kwa mfumo wa kuiwajibisha Serikali,
wananchi wanahitaji wafahamu wabunge wanatakiwa kuunda kamati nzuri ya
kukagua hesabu za serikali,”alisema Zitto.
Kwa upande wake Mbatia alisema ripoti za CAG
zimekuwa zikiibua madudu yanayofanya Serikalini lakini hakuna mhusika
anayechukuliwa hatua yoyote. Akitolea mfano, alisema kuwa fedha
zilizotajwa na CAG kupotea mwaka zikigawanywa kila mstaafu anayeidai
Serikali angelipwa Sh800, 000.
Mbatia alisema ‘dawa’ ya kuidhibiti serikalini
bungeni ni kwa kuhakikisha kuwa hakuna chama kinachokuwa na zaidi ya
asilimia 40 ya wabunge wote. Alisema kwa kufanya hivyo, wabunge watakuwa
na nguvu ya kutoa maamuzi ya pamoja.
“Jiulize kwanini mapato yasiyo ya kodi yanazidi
kushuka wakati bajeti inazidi kuongezeka. Hakuna nidhamu ya matumizi,
hii ya kutengeneza bajeti ni kuwadanganya Watanzania,” alisema Mbatia.
“Nafikiria kwa hali ilivyosasa tuweke watu ambao
si wala rushwa na kupunguza nguvu ya CCM. Ndani ya Bunge watu wanapokea
rushwa hawawezi kutekeleza ripoti ya CAG,” alisema Makaidi na kuongeza
kuwa hata bajeti zinazoandaliwa bungeni huanza ‘kutafununwa’ siku ya
pili baada ya kupitishwa kutokana na kukithiri kwa rushwa.
Akitumia dakika zake tatu kuelezea msimamo wa chama chake kuhusu
ripoti za CAG, Profesa Lipumba alisema kuwa pamoja na Rais Jakaya
Kikwete kunyooshewa kidole kwa kushindwa kutekeleza mambo kadhaa,
anampongeza kwa kufanikiwa kuimarisha ofisi ya CAG.
“Jambo kubwa sasa ni kwa taarifa hizo kufanyiwa
kazi. Katika kesi za Escrow kuna makosa ya wazi, lakini mpaka sasa watu
hawajawajibishwa,” alisema Profesa.
Kuhusu ajira
Pia, viongozi hao wa vyama waliulizwa watatumia
mikakati gani kupunguza tatizo la ajira nchini iwapo watapewa ridhaa na
wananchi kuongoza nchi.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa ndiye
aliyekuwa wa kwanza kujibu swali hilo kwa kusema kuwa sekta binafsi
ikishirkiana na Serikali ina nafasi kubwa kuhakikisha kuwa ajira
zinapatikana.
Suala la kuwapa wazawa nafasi ya kwanza
liliibuliwa na Dk Makaidi, aliyesema kuwa sera ya vijana inapaswa kuweka
kipaumbele kwa wazawa kwa kuwa kufanya hivyo siyo kuhubiri ubaguzi.
Kwa upande wake mtaalam wa uchumi, Profesa Lipumba
alisema chama chake kitatumia fursa ya kijiografia iliyopo nchini kwa
kuhakikisha bandari zinatumika vizuri kuhudumia nchi jirani na hivyo
kuongeza ajira kwa wananchi.
Zitto, alisema itakapofika mwaka 2030 Tanzania itakuwa na vijana milioni 36, na ongezeko hilo linahitaji kufanyiwa maandalizi.
0 comments :
Post a Comment