Warioba: Wagombea urais acheni tambo

  Hakuna mwenye uhakika na sifa walizozitaja
  Kazi ya kuwatambua waachiwe wananchi
Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba akizungumza katika mkutano wa Uzinduzi wa Uhuishaji Maadili ulioandaliwa na Chama cha Wataalamu wa Kikristo uliofanyika katika ukumbi wa Msimbazi jijini Dar es Salaam jana.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, amewaonya
makada waliochukua fomu za kuwania urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuacha tambo kwa kujitambulisha kwamba ni waadilifu, badala yake kazi ya kuwatambua waachiwe wananchi.

Akizungumza wakati akizindua kampeni ya uhuishaji wa maadili jijini Dar es Salaam jana, Jaji Warioba alisema kati ya wagombea wote hakuna mwenye uhakika kama ana sifa hizo walizozitaja.

Mpaka sasa makada zaidi ya 30 wa chama hicho wametangaza nia na kuchukua fomu ya kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais kupitia CCM.

Jaji Warioba alizindua Kampeni hiyo inayoitwa Vuguvugu la uhuishaji maadili, imeandaliwa na Umoja wa Wanataaluma wa Kikatoliki nchini (CPT) yenye lengo la kurudisha uadilifu kwa Watanzania baada ya kuonyesha ishara ya kutoweka.

Alisema kitu kinachompa wasiwasi ni baadhi ya wagombea kujinadi hadharani kwamba wana sifa za uadilifu, kitu ambacho hakifai.

“Nashangazwa na hatua za baadhi ya watu wanaotia nia ya urais kujinadi mbele ya umma eti wao ni waadilifu, jambo hilo hawapaswi kusema wao wenyewe, watuachie wananchi tunajua nani ana sifa ya uadilifu kwa sababu ndiyo tunawajua,” alisema Jaji Warioba.

Alisisitiza kwamba kazi ya kuwachambua nani msafi na nani anafaa kushika nafasi hiyo inabaki kwa Watanzania ambao wanafahamu mgombea gani anatoa rushwa na nani hatoi.

Alisema Tanzania imeshuhudia kipindi kigumu cha mmomonyoko wa maadili, ambapo vitendo vya rushwa vimetawala na kusababisha kuibuka kwa matabaka ya wachache walionacho na wengi wakiishi katika umasikini wa kutupwa.

Jaji Warioba ambaye amewahi kushika nafasi mbali mbali za uongozi tangu Serikali ya Awamu ya Kwanza na hatimaye kuwa Waziri Mkuu, alisema katika kuliona hilo, kwenye rasimu ya Katiba Mpya, waliweka misingi ya nchi inayokataza viongozi kupokea zawadi, kuweka fedha nje ya nchi na kujihusisha na biashara.

“Huwezi kuwa kiongozi kama umeweka pesa nje au kupokea zawadi binafsi, tuliweka hivyo kwa maana nzuri tu kwamba mtu asijinufaishe binafsi kwa mali ya umma,” alisema jaji Warioba.

Warioba pia alitaka suala la maadili lijengwe kuanzia ndani ya jamii kwa sababu huo ndio msingi mkuu wa uongozi katika kujenga utaifa na uzalendo, Lazima kuwa na misingi ya kuwatambulisha Watanzania, kwa kuweka tunu ya taifa.

“Hata wananchi walizungumzia kwa uzito sana suala hili, tuliwasikiliza  na tulichukua uamuzi wa kuhakikisha kuwapo kwa tunu za Taifa ambazo ni msingi wa kujenga maadili,” alisema.

Alizitaja tunu hizo ambazo zilikataliwa na wajumbe wa Bunge maalum kuwa ni utu, uzalendo, uwazi, wajibikaji na Lugha ya Taifa.

Alisema viashiria vinavyoonekana vya kuporomoka kwa maadili kuna hatari ya amani, umoja na mshikamano vinatoweka.

“Siyo siri ubaguzi wa kidini, kikabila, rangi unaanza kuonekana. Ubaguzi mpya umeibuka ambapo ni wa vyama vya kisiasa, mtu akivaa nguo za kijani na ukaonekana kwenye mkutano wa kombati utaanza kuitwa msaliti na kusongwasongwa,” aliongeza kusema.

Awali, Profesa Beda Mutagahywa, alisema kwa miongo kadhaa misingi ya umoja na mshikamano umetetereka na kupata nyufa zinazotishia amani ya nchi.

Alisema uadilifu wa watu umepotea ambapo kwa hivi karibuni kumejitokeza kashfa nyingi zilizowahusisha watumishi wa umma na watawala kuchukua rushwa na  uvunjaji wa haki za binadamu lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.

Profesa Mutagahywa alisema kwa kutumia kampeni hiyo, watatumia njia ya majadiliano ya kina ndani ya jamii katika kujenga jamii mpya inayofuata misingi ya utu, uwajibikaji na upendo kwa kila mtu.

Naye Askofu Mkuu Paul Ruzoka wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora, alisema kuporomoka kwa maadili kwa baadhi ya watu waliopewa mamlaka ni dalili ya watu kutokuwa na hofu ya Mungu.

Alisema jamii inatakiwa kurudi nyuma na kuanza upya ujenzi wa Taifa kwa kuweka mbele umoja na mshikamano.

“Neno uadilifu ni dalili ya uwepo wa Mungu, mtu akiwa na sifa hizo anafanya wajibu wake kwa maslahi ya umma, lakini kwa sasa tunashuhudia watu hawana hofu wanaweka mbele ubinafsi,” alisema Askofu Ruzoka.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment