Urais 2015: Mafuriko ya Lowassa Yatua Manyara....... Azoa Wadhamni 42,405

Friday, June 26, 2015

Nkupamah blog

Mbunge wa Babati Mjini (CCM),  Kiseryi Chambiri, amesema anamuomba Mungu jina la Waziri Mkuu wa zamani,  Edward Lowassa liwe ni miongoni mwa majina matatu ya wagombea urais yatakayofika katika Mkutano Mkuu wa CCM kwani litakapoonekana watakuwa wamemaliza kazi na uchaguzi.

Kauli hiyo aliitoa jana katika uwanja wa Old Majengo wilayani Babati wakati wa kukabidhi wanachama wa CCM waliojitokeza kumdhamini Lowassa katika mbio zake za kusaka urais kwa tiketi ya chama hicho. Katika Mkoa huo alipata jumla ya wadhamini 42,405.

Chambiri alisema safari ya Lowassa ni ndefu lakini karibu wanafika mwisho na anachoomba katika majina matatu yatakayofika katika himaya yao kama wajumbe wa Mkutano huo jina lake liwemo kusudi waweze kufanya kazi.

“Kwa sababu kwa mujibu wa taratibu za CCM majina yale matatu huletwa ili yaweze kupigiwa kura, kama jina lako halipo hatuwezi kufanya kazi na mimi nakuombea kwa mungu basi katika yale majina matatu yatakayoletwa kwaajili ya kupigiwa kura na lako liwepo,” alisema Chambiri.

Alisema  endapo jina hilo litakuwapo watakuwa wamemaliza kazi na uchaguzi utakuwa umemalizika.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha Onesmo Nangole, alisema matumaini yaliyopo ni makubwa kwani Lowassa ni mtu mkarimu na mpole na chakula chake huliwa na masikini na mtu mwenye nywele nyeupe anautukufu.

Akizungumza na wanachama na wananchi, Lowassa aliwashukuru kwa kujitokeza kumdhamini na kusema imani huzaa imani na kwamba atahakikisha akipata nafasi hiyo atawatumikia.

“Nawashukuru kwa wale walionidhamini najua CCM wanahitaji wachache lakini nimedhaminiwa na wengi, nitaenda kuyahifadhi nyumbani kwangu kama kumbukumbu na historia ya maisha yangu nasema nashukuru sana,” alisema Lowassa.

Aidha alisema wakimchagua wahakikishe wanapenda kuchapa kazi maana anataka kuendesha nchi mchakachaka ili  kuondokana na umasikini.

Aliwawakumbusha kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kupigia kura kwani ni haki yao ya msingi na kikatiba.

“Natamani niongee mengi lakini kanuni haziruhusi ibaki kusema naomba muendelee kuniombea katika hili na nina wapenda sana,” alisema Lowassa.

Awali Katibu wa CCM Wilaya ya Babati, Daniel Ole Porokwa, alisema wanachama wa CCM 42,405 wamejitokeza kumdhamini Lowassa katika mkoa huo tofauti na wengine waliodai hatapata wadhamini wengi Manyara.

“Waliokudhamini wote wamejitolea na ndiyo maana wapo hapa, haya ni mapenzi tu ya wananchi na naamini wewe ndio utakayekuwa Rais wa Tanzania…Hakatwi mtu hapa,”alisema.

Alisema katika wilaya ya Mbulu wamemdhamini 9,500, Babati Mjini 12,500, Babati Vijijini 6,000, Hanang' 5,700, Kiteto 5,550 na Simanjiro 10,300.



Nkupamah blog
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment