
Kauli hiyo ya Jaji Warioba imekuja wakati mgombea huyo akipokewa Dar es
Salaam leo akiambatana na mgombea mwenza wake, Samia Suluhu Hassan
katika mkutano wa kuwatambulisha kwa wananchi utakaofanyika Mbagala
Zakhiem.
Juzi, Magufuli alipitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM kwa kura 2,104 na
kuwashinda Balozi Amina Salum Ali aliyepata kura 253 na Dk Asha Rose
Migiro kura 59.
Jaji Warioba ambaye awali aliwakemea baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo
ndani ya CCM kwa kukiuka kanuni, alisema mchakato huo ulikuwa
umeingiliwa na kila aina ya michezo michafu ya rushwa na uvunjaji wa
kanuni na taratibu, lakini alielezea kufurahishwa kwake baada ya mambo
hayo kuwekwa kando wakati wa kupitisha mgombea.
“Nilikuwa na wasiwasi kama vikao vya chama vitatenda haki katika
kupitisha mgombea kutokana na baadhi ya viongozi kujipambanua wazi kwa
wagombea wanaowaunga mkono,” alisema Jaji Warioba jana.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Jaji Warioba alieleza kasoro mbili zilizoibuka
katika mchakato huo, moja ikiwa ni baadhi ya wagombea kueleza sera zao,
wakati wakijua wazi kuwa sera za CCM ziko kwenye ilani yake ya uchaguzi
na pili, kukiukwa kwa utaratibu uliowekwa na chama hicho kwamba yeyote
anayehusika kwenye ngazi ya uamuzi, asimdhamini mgombea yeyote wa urais.
Mbali na Warioba ambaye ni Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba, jambo hilo pia lilikemewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku na wajumbe wa iliyokuwa tume hiyo katika
kongamano lililoandaliwa na taasisi hiyo lililofanyika Julai 9, Dar es
Salaam.
“Nimefarijika jinsi hali ilivyokuwa nadhani kwa mara ya kwanza fedha
haikushinda,” alisema Jaji Warioba huku akisisitiza kuwa ni jambo baya
kumpata kiongozi kwa nguvu ya fedha.
Alisema pamoja na kuwa fedha haikushinda, lakini ukweli ulio wazi ni
kwamba wapo waliotumia fedha nyingi katika mchakato huo kwa lengo na
kupitishwa kugombea urais.
“Sote tunajua kuwa Magufuli hakutumia fedha wala viongozi wakati akisaka
wadhamini mikoani. Yeye alikwenda kwa wanachama na kutafuta wadhamini
kimyakimya. Ni mtu sahihi. Alifanya kazi hiyo bila kutumia fedha,”
alisema.
Alisema makundi yalikuwa yanatishia kuvunja umoja ndani ya chama hicho
na kwa sasa ana imani na Dk Magufuli kuwa atawaunganisha wanaCCM
kutokana na rekodi zake za utendaji kazi.
Alisema mbunge huyo wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi ni chaguo
zuri kwa kuwa si mtu wa makundi na atakuwa na kazi nyepesi kuwaunganisha
wanachama wa CCM.
Viongozi wa dini walonga
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania,
Sheikh Khamis Mataka alisema CCM imefanikiwa kumpata mgombea makini
ambaye hana makundi wala kashfa za rushwa.
Sheikh Mataka alisema uteuzi wa Dk Magufuli ni tumaini jipya kwa
Watanzania kwa sababu amejipambanua kwa utendaji wake wa kazi serikalini
ikiwa ni pamoja na kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Nakumbuka kulikuwa na mfanyabiashara mmoja ambaye alitaka kusafirisha
boti kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kwa njia ya barabara, Dk
Magufuli alimzuia kwa sababu barabara hazihimili uzito mkubwa,” alisema.
“Hakuna aliyedhani kuwa Magufuli atakuwa mgombea urais wa CCM,
alichukua fomu kimyakimya, alitafuta wadhamini kimyakimya, alirudisha
kimyakimya,” alisema Sheikh Mataka.
Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Ngara mkoani Kagera, Severini
Niwemugizi alipongeza uteuzi wa Dk Magufuli kwa kuwa amekuwa mtendaji
kazi na amekuwa akitenda haki kulingana na taratibu za kisheria.
Hata hivyo, Askofu Niwemuguzi alisema hana imani na mgombea mwenza,
Samia kutokana na utendaji wake akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la
Katiba.
Alisema kuwapo makamu wa rais aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bunge hilo
haoni kama Watanzania watapata matumaini ya kupata katiba waitakayo kwa
masilahi ya Taifa.
“Labda wapate ushauri mzuri wanaweza kuafikiana na kurudisha mchakato wa
Katiba Mpya na kutuunganisha na kubaini chanzo cha kutugawa kutokana na
Katiba Inayopendekezwa,” alisema.
Alishauri, iwapo Dk Magufuli atashinda asimamie maendeleo ya wananchi
kwa kuweka mikakati ya kuboresha elimu ambayo inaweza kuinua maisha ya
Watanzania dhidi ya umaskini
“Elimu ndiyo itaondoa maradhi na umaskini na watu kutumia fani
mbalimbali katika mazingira yao kujikwamua kiuchumi,” alisema Askofu
Niwemugizi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania
(TEC).
Mapokezi Dar
Akizungumzia mapokezi ya mgombea huyo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dar
es Salaam, Juma Simba alisema Dk Magufuli na Samia watapokewa saa 8.00
mchana wakitokea Dodoma.
Simba alisema mkutano huo ambao utahutubiwa na wagombea hao wawili,
utawakutanisha wanaCCM na wananchi kutoka katika wilaya za Ilala, Temeke
na Kinondoni.
“Lengo la mkutano huo ni kuwatambulisha na kuwapongeza wagombea hao
watakaopeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu,” alisema.
Simba alisema kwa kumteua Magufuli, mgombea yeyote atakayesimamishwa na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania urais atashindwa.
Chavita wampongeza
Uteuzi wa Dk Magufuli umepokewa kwa mikono miwili na watu wenye ulemavu
wa kusikia mkoani Morogoro kutokana na utendaji wake na kutokuwa na
makundi ndani na nje ya chama.
Katibu wa Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) mkoani Morogoro, Henry
Matasia alisema uchapakazi wa Dk Magufuli ndiyo uliowafanya wamkubali na
kuwa na imani naye tofauti na kama angeteuliwa mtu mwingine.
Pia, wafanyabiashara wa Soko la Mawenzi, John Peter na Tatu Bakari
walisema Dk Magufuli ni kiongozi anayekubalika na wananchi katika
utendaji wake.
Dk Shein apokewa Zanzibar
Katika hatua nyingine, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Dk Ali Mohamed Shein
jana alipokewa Zanzibar kwa kishindo baada ya kuteuliwa tena kugombea
urais wa Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman Karume,
Dk Shein alisema mchakato wa kumpata mgombea urais wa Muungano kupitia
CCM haukutawaliwa na sintofahamu yoyote kama baadhi ya watu
wanavyoeleza, bali ulizingatia utaratibu na kanuni za uchaguzi za chama
hicho. “Tulijadili kwa kina sifa za wagombea na kushauriana hadi
mwishoni tukafikia makubaliano na ndiyo maana tulipiga kura kwa utulivu
na nidhamu kwa mujibu wa taratibu za chama chetu,” alisema Dk Shein.
Kuhusu malalamiko kuwa baadhi ya wananchi wananyimwa vitambulisho vya
ukaazi na hatimaye kukosa kupiga kura, Dk Shein alieleza kushangazwa na
baadhi ya wanasiasa kuwapotosha wananchi kwa kutaka suala hilo
lishughulikiwe kisiasa badala ya kufuata sheria zilizopo.
“Baadhi ya wanasiasa wanajisahau na kuwapotosha wananchi. Sheria
haikusema wanasiasa washughulikie matatizo ya vitambulisho badala yake
imeelekeza wananchi wafanye hivyo kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Raymond Kaminyoge, Peter Elias (Dar), Esther Mwimbula (Morogoro) na Shaban Ndyamukama (Ngara).
Mwananchi


0 comments :
Post a Comment