Licha ya kuwa siasa ni pata potea, kwa wanasiasa vijana huenda mchakato
huo ukawa ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye kilele cha mafanikio na
kwa baadhi ya vigogo huenda ukawa ndiyo mwanzo wa kuelekea kustaafu
siasa.
Edward Lowassa, Frederick Sumaye, Dk Mohammed Gharib Bilal, Stephen
Wasira, Mizengo Pinda, Samuel Sitta na Profesa Mark Mwandosya ni makada
waliojitokeza kujaribu bahati yao ya kuteuliwa kugombea urais, lakini ni
dhahiri kuwa sasa watakuwa wanaanza kujiwekea mazingira ya kuachana na
siasa.
Wote hawakumudu kuingia kwenye orodha ya wagombea watano waliopelekwa
kwenye Halmashauri Kuu kwa ajili ya kuchujwa hadi kubakia watatu ambao
hupelekwa kwenye Mkutano Mkuu kwa ajili ya kumpata mgombea urais wa CCM.
Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM wa kumuachia mteule agombee kwa vipindi
viwili iwapo anashinda uchaguzi wa Rais, makada hao sasa watalazimika
kusubiri hadi mwaka 2025 ili kujaribu tena bahati yao, jambo ambalo
linaonekana halitakuwa rahisi.
“Nyakati za kisiasa zinabadilika haraka sana. Miaka 10 ijayo siyo
mchezo,” alisema Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Hamad
Salim alipohojiwa na Mwananchi kuhusu mustakabali wa makada waliokosa
nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
“Kwa kipindi hicho, mambo mengi yatabadilika, wanasiasa waliogombea
kipindi hiki hawawezi kuwa kwenye umaarufu wa sasa, wanaweza kupanda
chati au kushuka.
“Pia, kuna suala la umri wazee kama Dk Bilal au Sumaye miaka 10 ijayo
kupanda jukwaani na kushuka mara kwa mara itakuwa shida kidogo.
Wanasiasa wengi waliokuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho ni wazee na ule
siyo umri wa kushinda majukwaani.”
Licha ya sifa za mgombea kutozungumzia umri wa juu bali wa chini ambao
ni kuanzia miaka 40, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Richard
Mbunda alishauri baadhi ya vigogo walioshindwa kupumzika kupisha damu
changa za mabadiliko.
Alisema: “Siasa nchini hazitabiriki na ni za kipekee kwani unaweza ukawa
maarufu usichagulike na siku zinavyokwenda ukapoteza umaarufu huo.
“Kwa hali ya sasa, Bilal, Pinda, Lowassa, Sitta tayari walishakamata
nafasi za juu nchini na umri wao umeshasogea. Bila shaka ni muda muafaka
kupisha wengine… wameshaitumikia nchi vya kutosha na wana marupurupu ya
kutosha baada ya kustaafu. Ni bora wawaachie vijana walete mabadiliko,”
alisema Mbunda.
Alisema makada hao ni washauri wazuri iwapo wataachana na siasa za
kushindana. Alisema hata kwa wale ambao umri unawaruhusu, haitakuwa
vizuri kuwapa vyeo vidogo kama vya ubalozi na kwa maana hiyo alisema
safari yao kisiasa, imefikia ukingoni.
Mchakato huo wa urais wa CCM ulitawaliwa na jina la Lowassa, ambaye
alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuteuliwa baada ya harakati zake za
kusaka wadhamini kuhudhuriwa na maelfu ya watu kuthibitisha kauli ya
Rais Jakaya Kikwete kuwa chama hicho kingechagua mtu anayekubalika ndani
na nje ya CCM.
Lakini hakumudu kuingia tano bora na hivyo kuacha mgogoro mkubwa
uliosababisha wajumbe wa Halmashauri Kuu kumuimbia Kikwete wimbo
ulioonyesha kuwa wana imani na mbunge huyo wa Monduli.
Majeraha kwa waziri huyo mkuu wa zamani, pia yanaonekana kwenye kauli
ambazo zimekuwa zikitolewa na Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alikuwa
mstari wa mbele kumnadi na ambaye ameeleza wazi kuwa viongozi wa CCM
walikula njama kumuengua.
Lowassa (62) pia alijitosa kwenye mchakato huo mwaka 1995 alipokwenda
kuchukua fomu pamoja na Kikwete, lakini jina lake likaenguliwa.
Dk Bilal
Kada mwingine anayeonekana kuachwa akiwa na majeraha makubwa ni Dk
Bilal, ambaye ni Makamu wa Rais. Bilal amepoteza nafasi ya kuendelea
kushika nafasi hiyo baada ya mteule wa CCM, Dk John Magufuli
kumpendekeza Samia Salim Suluhu kuwa mgombea mwenza. Kwa makamu wa Rais
kutoingia tano Bora ni pigo kubwa.
Dk Gharib (70) aligombea urais wa Zanzibar mwaka mwaka 2010 na
kushindwa, lakini CCM ikamteua kuwa mgombea mwenza wa Kikwete baada ya
Dk Mohamed Shein kuteuliwa kugombea urais wa Zanzibar. Atakuwa akiuguza
majeraha kwa kuwa mtu wa kwanza kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi
kimoja tangu siasa za ushindani zirejeshwe nchini.
Membe
Kundi lililoachwa na majeraha pia linamjumuisha Membe, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambaye ameaga sehemu mbalimbali
alizokuwa zikimhusu kutokana na kazi yake ya kisiasa na hasa jimboni
kwake ambako tayari Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye ameshachukua
fomu.
Membe (62) amefanya wizara hiyo kwa takriban miaka minane na alikuwa
mmoja wa makada waliokuwa wanapewa nafasi kubwa. Alipenya kwenye tano
bora, lakini akashindwa vibaya kwenye kura za wajumbe wa Halmashauri Kuu
na sasa atakuwa akitafakari upya hatma yake kisiasa.
Pinda
Waziri Mkuu, Pinda naye ameachwa na majeraha. Ameingia kwenye orodha ya
watu walioshika cheo hicho na ambao wamejaribu kuwania urais na
kuenguliwa mapema.
Machungu ya kuenguliwa Pinda (67) pia yanatokana na ukweli kuwa alikuwa
mtendaji mkuu wa Serikali na hivyo ilikuwa rahisi kushauriwa
kutojiingiza kwenye mchakato kama hakuwa na nafasi hata ya kuingia tano
bora.
Mbunge huyo wa Katavi ameshatangaza kuachia jimbo hilo na baada ya
matokeo hayo, mustakabali wake utategemea busara ya viongozi wa Serikali
ya Awamu ya Tano.
Profesa Mwandosya
Mchakato huo pia umeacha jeraha katika jaribio la pili la Profesa
Mwandosya, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), la
kuwania urais baada ya mwaka 2005 kushika nafasi ya pili nyuma ya
Kikwete aliyeongoza na Dk Salim Ahmed Salim.
Profesa Mwandosya, kama baadhi ya makada walioenguliwa, ameshatangaza
kutogombea ubunge Jimbo la Rungwe Mashariki, hali ambayo imesafisha njia
ya kuelekea kustaafu siasa baada ya kushindwa kwenye mbio za urais.
Sitta
Spika huyo wa Bunge la Tisa na pia Mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
anaingia kwenye orodha ya majeruhi wa mchakato wa urais wa CCM baada ya
kujiandaa kwa muda mrefu kuwania nafasi hiyo.
Sitta alisema bayana wakati alipochaguliwa kuongoza chombo hicho cha
kihistoria cha kuandika Katiba kuwa atatumia uspika wake kutengeneza
mazingira ya kuteuliwa na CCM kugombea urais.
Lakini naye hakupenya hata kwenye tano bora na inaelekea hatua inayofuata ni kwenda Tabora kutetea jimbo lake.
Akiwa na umri wa miaka 73, mwanasiasa huyo mkongwe sasa hana nafasi ya
kugombea tena urais baada ya miaka 10 atakapokuwa na umri wa zaidi ya
miaka 80.
Sumaye
Waziri Mkuu huyo wa Serikali ya Awamu ya Tatu, atakuwa akiuguza majeraha
ya kupoteza nafasi ya kuteuliwa kwa mara ya pili baada ya jaribio lake
la kwanza mwaka 2005 kugonga mwamba.
Alishaachana na siasa za majimbo tangu mwaka 2005 baada ya kukosa urais
na akiwa na umri wa miaka 65, haiyumkini kuingia tena kwenye mbio za
urais mwaka 2025.
Wasira
Waziri huyo wa Kilimo, Chakula na Ushirika, alitangaza awali kuwa
asingegombea ubunge wa Bunda, lakini akabadilisha uamuzi huo licha ya
kuingia kwenye mbio za urais. Wasira, ambaye mwaka huu ametimiza miaka
70, atakuwa akiwania kurejea bungeni akipambana na mwanasiasa kijana
ndani ya CCM, Esther Bulaya.
“Ni wazi kwa waliokuwa na matumaini makubwa ya kushinda ni pigo sana
kuangushwa. Hata matamshi yao yalikuwa wazi kuwa walikuwa na uhakika
hata walidiriki kusema ‘jina langu halitakatwa’ na mbio zao za kutafuta
wadhamini zilikuwa ni za kishindo,” alisema Profesa Gaudence Mpangala,
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco).
Profesa huyo wa masuala ya siasa na utawala, alisema kwa hali ya kawaida
wagombea hao wameathirika kisaikolojia, hivyo hata wale waliokuwa
wametangaza kutogombea wanaweza kubadili msimamo na kurudi kutetea
majimbo yao.
“Magufuli akipata urais anaweza kuwafikiria hata uwaziri na iwapo
upinzani watashinda, hali yao kisiasa ndiyo basi tena. Siasa siyo kazi
ya kudumu, bali ni ya muda tu wa kuwatumikia wananchi ukimalizika,
unastaafu.”
MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment