Monday, November 9, 2015
@nkupamah blog
Baraza
la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limetoa saa
72 kwa Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HELSB) kuhakikisha inawapa mikopo wanafunzi wote waliobaki wa Vyuo
Vikuu na wakishindwa kufanya hivyo wataitisha mgomo nchi nzima.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa BAVICHA,
Julias Mwita, alisema Serikali ya CCM iliamua kuiga ilani ya CHADEMA
bila kujipanga na matokeo yake wanafunzi wa Elimu ya Juu zaidi ya
asilimia 82 wamekosa mikopo.
Alisema
wanafunzi wengi waliokosa mikopo wanatoka katika familia maskini jambo
ambalo haliwezi kukubalika hivyo wao wameshafanya maandalizi yote ya
migomo kwa wanafunzi wote waliokosa mikopo nchi nzima hivyo
wanachosubiri ni kumalizika saa 72 walizotoa kama jambo hilo
lisipotekelezwa wachukue hatua.
"Sisi
tuna mitandao ya wafunzi wa Elimu ya Juu nchi nzima, licha ya kufanya
mgomo tutawafundisha njia nyingine ya kudai haki yao bila uvunjifu wa
amani... mimi nilikwenda rumande siku tisa tangu Oktoba 25, mwaka huu,
nilikuwa naongoza kundi la watu 40 kukusanya matokeo ya Uchaguzi Mkuu
nchi nzima.
"CCM
nao walikuwa wakifanya hivyo pale Mlimani City na Golden Tulip lakini
cha ajabu, sisi ndio tuliokamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kusambaza
taarifa wakati wenzetu walikuwa wakifanya kazi kama hiyo," alisema Mwita.
Aliongeza
kuwa, aliyekuwa mgombea urais wa CHADEMA anayeungwa mkono na vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), Edward Lowassa
alidhalilishwa kwa kutukanwa kila aina ya matusi na viongozi wa CCM na
wengine walifikia hatua ya kusema hawaiachi Ikulu au kukabidhi nchi kwa
makaratasi.
"Pamoja
na maneno haya kuzungumzwa na wana CCM, hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa na polisi lakini ingekuwa sisi, tungekuwa rumande," alisema.
Kwa
upande wake, Mratibu wa Uhamasishaji Taifa wa BAVICHA, Edward Simbeye,
alisema wao wanaamini aliyekuwa mgombea wao wa urais alishinda lakini
ameporwa ushindi wake.
"CCM
wana Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu ambao na wao wamekosa mikopo,
wanafunzi wote waliokosa mikopo wataandamana hadi Bodi ya Mikopo kutoka
nchi nzima kwani hili ni jambo kubwa lisiloweza kufumbiwa macho," alisema.
0 comments :
Post a Comment