Monday, November 30, 2015
@nkupamah blog
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Konondoni, kimempitisha Diwani mteule wa Ubungo, Boniface Jacob (Chadema), kuwa mgombea umeya wa Manispaa ya Kinondoni, huku akiwakilisha mwamvuli wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mgombea
huyo alikuwa akiwania nafasi hiyo huku akipambana na diwani mwenzake
mteule wa Kata ya Mbweni, Abdunel Elibariki (Chadema) ambaye alishindwa
kutamba.
Akitangaza
matokeo ya uchaguzi huo jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa
uchaguzi huo Venus Kimei , alisema Jacob alishinda kwa kura 20 kati ya
kura 28 zilizopigwa.
“Wagombea
walikuwa wanne lakini watatu ndio ambao walikidhi vigezo, hata hivyo
waliopigiwa kura ni wawili kutokana na mgombea mmoja Ndeshukurwa
Tungaraza ambaye ni Diwani mteule wa Kata ya Makongo kujitoa katika
hatua za mwisho,” alisema.
Akizungumza
baada ya kutangazwa kushinda kinyang’anyiro hicho, Jacob alisema ana
imani atashinda katika uchaguzi utakaowajumuisha wagombea wa vyama
vingine kikiwamo Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Nitasimamia
kwa vitendo sera ya elimu ambayo chama chetu iliisimamia katika kampeni
na jambo zuri ni kwamba hata Rais Dk. John Magufuli amesisitiza kwamba
watoto wasome bure kuanzia msingi hadi sekondari.
“Hivyo
ninaamini hilo linawezekana endapo tutasimamia mapato ya ndani kwa
umakini nataka Manispaa Kinondoni iwe mfano katika hili ambayo
tutahakikisha tunaboresha maslahi ya walimu na kuondoa kabisa michango
ya aina zote,” alisema.
Alisema
atasimamia kwa kuzingatia sera ya utatu akijumuisha wananchi, wanasiasa
na wataalam bila kuwabagua kwani kwa pamoja watainua maendeleo ya
manispaa hiyo.
Kwa
upande wa Chama cha Wananchi (CUF), ambacho ni mshirika wa Ukawa,
kinatarajia kumsimamishwa Diwani mteule wa Kata ya Tandale, Jumanne
Mbunju (CUF) ili awanie nafasi ya unaibu meya wa manispaa hiyo.
Katika
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni yenye majimbo manne, Chadema
imenyakua majimbo matatu ambayo ni Ubungo, Kawe na Kibamba, huku jimbo
moja la Kinondoni likienda CUF.
Kata
zinazounda halmashauri hiyo ni 34 ambapo Chadema ilishinda kata 18 na
kupata madiwani wa viti maalumu 7, CCM kata 11 na viti maalumu 4 na CUF
ikishinda kata 5 na viti maalumu 2.
0 comments :
Post a Comment