@nkupamah blog
Marekani
imeiweka njiapanda Serikali ya Rais Dk. John Magufuli, baada ya Bodi ya
shirika lake la Changamoto za Milenia (MCC) kuamua kukutana kesho
kujadili masuala kadhaa ya utoaji wa misaada kwa nchi zinazoendelea huku
angalizo lake kwa serikali ya Tanzania kuhusiana na uchaguzi wa
Zanzibar likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi.
Kwa
mujibu wa ratiba ya MCC, kikao chao cha Bodi kitakutana kesho
(Jumatano) na kupitia mapendekezo ya kupeleka misaada kwa nchi
mbalimbali zinazoendelea.
Inaelezwa kuwa kikao hicho kitafanyika kwenye ukumbi wa Holbrooke, saa 4:00 asubuhi kwa saa za Marekani.
Inatarajiwa
kuwa kupitia kikao hicho, nchi zitakazokidhi vigezo zitakuwa na fursa
ya kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya
maendeleo iliyojipangia yenyewe kabla ya kupata fedha hizo.
Tanzania inasubiri kuidhinishiwa fedha za awamu ya pili za MCC Dola za Marekani milioni 472 (takribani trilioni moja).
Hata
hivyo, kutokana na ratiba hiyo, Serikali ya Rais Magufuli inatarajiwa
kuwa njiapanda kwani suala la Zanzibar lililokumbushiwa na MCC kupitia
maelekezo yake yaliyoripotiwa mwezi uliopita, bado linaonekana kuwa
kuendelea kuwa tete.
Hadi
sasa, licha ya vikao mbalimbali vinavyoendelea kufanyika na
kuwakutanisha wagombea waliokuwa wakichuana kwa karibu kabla ya uchaguzi
huo kufutwa, Dk. Ali Mohamed Shein wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na
Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), bado ufumbuzi
haujapatikana.
CCM
wanaamini kuwa uchaguzi huo ni lazima urudiwe baada ya kufutwa na
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, huku
CUF wakisisitiza kuwa uchaguzi huo haukuwa na kasoro kubwa kiasi cha
kufutwa wote na hivyo kutaka matokeo yatolewe na mshindi atangazwe kuwa
Rais wa visiwa hivyo.
Awali,
katika angalizo lake kwa serikali ya Magufuli iliyoingia madarakani
Novemba 5, 2015, MCC ilitaka kupatiwa ufumbuzi kwa suala la Zanzibar na
pia kuwapo kwa ufafanuzi juu ya watuhumiwa waliokamatwa kwa makosa ya
mtandao wakati wa Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25.
Ilifahamika
kuwa maelekezo ya MCC kwenda kwa mamlaka mbalimbali za serikali ya
Tanzania, yalionyesha kuwa lipo tishio la kufutwa kwa msaada huo
(trilioni moja) iwapo mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar hautapatiwa
ufumbuzi na pia kutolewa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya mtandaoni
kabla ya kikao cha bodi ya MCC mwezi huu (Desemba, 2015).
“MCC
inafuatilia kwa karibu hatua zitakazochukuliwa na serikali ya Magufuli
katika suala la utawala bora, katika kipindi hiki tunapokaribia kufanya
kikao cha bodi ya MCC Desemba. Utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar kwa
kuridhisha pande zote zinazohusika,” ilielezwa katika kile kilichodaiwa kuwa ni sehemu ya angalizo la MCC kwa serikali ya Tanzania na kuripotiwa Novemba, 2015.
Katibu
Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliwahi kulitolea ufafanuzi suala
hilo Novemba 29, 2015, akisema kuwa Serikali haina wasiwasi kuhusu
mashariti ya MCC juu ya Zanzibar kwani yatafanyiwa kazi kabla ya bodi ya
MCC kukutana tena (Desemba).
Hata
hivyo, hadi sasa hakuna muafaka uliotangazwa rasmi kuwa umefikiwa
kuhusiana na uchaguzi wa Zanzibar huku pande zote zikiendelea kutoa
msimamo tofauti; hali hiyo ikielezwa kuwa inaiweka njia panda serikali
ya Magufuli kwani fedha za MCC ni muhimu katika utekelezaji wa ahadi
zake mbalimbali, hasa juu ya dhamira ya kusambaza umeme na kuwaunganisha
wananchi wengi katika gridi ya taifa.
Kadhalika, fedha za awamu ya pili za MCC ni muhimu pia katika uimarishaji wa taasisi zinazohusika na sekta ya nishati.
Akizungumzia
hatari iliyopo sasa ya kukosa fedha za MCC baada ya suala la uchaguzi
wa Zanzibar kutopatiwa ufumbuzi, Balozi Sefue alisema hakuna hofu yoyote
(ya kukosa fedha) kwa sababu tayari kuna hatua kadhaa zimechukuliwa na
Serikali ya Tanzania kushughulikia mambo yaliyohojiwa na MCC.
Akieleza
zaidi, Balozi Sefue alisema taarifa ya MCC haikusema masuala hayo
mawili yaishe vipi, bali walieleza yashughulikiwe; na kwamba hivi sasa
yanaendelea kushughulikiwa na yanaendelea vizuri.
Alisisitiza kuwa Tanzania imefuata mashariti yote ya kupata fedha hizo kutoka MCC.
“MCC
walituambia sisi kama serikali kuwa yaangalieni masuala haya, na siyo
kwamba walituambia tuyashughulikie hadi tuyamalize ndipo watatupatia
fedha … hilo siyo kweli,” alisema Balozi Sefue.
Aliongeza
kuwa hadi sasa, hatua zilizofikiwa katika kutatua mgogoro wa Zanzibar
na pia suala la wahalifu wa makosa ya mtandao, yote hayawezi kuikosesha
sifa Tanzania kupata fedha hizo.
0 comments :
Post a Comment