Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Zuberi Samataba(katikati) akitoa
mwongozo jana juu ya suala la kufanya usafi kwa wakuu wa idara(hawapo
pichani) wa Halmashauri wa Manispaa ya Temeke. Wengine katika picha ni
Mkurugezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke Bw. Photidas Kagimbo
(kushoto) na Mkurugenzi wa Utumishi na Raslimali Watu wa TAMISEMI Bw.
Mohamed Pawaga(kulia)
Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) anayeshughulikia Elimu Bw. Zuberi Samataba akisisitiza juu ya
utekelezaji wa agizo la Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli la usafi wa mazingira ,jana wakati alipotembelea
Ofisi ya Msimamizi wa soko la Temeke Sterio lililopo katika Halmashauri
ya Manispaa ya Temeke.
Picha zote na Beatrice Lyimo -MAELEZO
………………………………………………………………………………………..
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es salaam
Serikali imewataka wananchi wote kuwajibika katika
usafishaji wa mazingira na maeneo yanayowazunguka ili kudhibiti magonjwa
mbalimbali ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)
anayeshughulikia Elimu Zuberi Samataba wakati wa ziara yake katika
Halmashauri ya Manispaa ya Temeke ya ukaguzi na utoaji mwongozo katika
kutekeleza agizo la Rais la kutumia siku ya Uhuru kufanya usafi.
Alisema kuwa kila mwanachi anapaswa kuhakikisha mazingira
anayoishi na yale yanayomzunguka yanakuwa safi wakati wote ili kupunguza
mlipuko wa kipindupindu.
Samataba alisema kuwa mazingira yanayowazunguka wananchi
yakiwa safi yatapunguza matumizi ya serikali yanatokana na ununuzi wa
dawa za kutibu wagonjwa wa kipindupindu na hivyo fedha hizo kuelekezwa
katika matumizi mengine.
“Kila mmoja akiwajibika mahali pa kazi na mazingira
yanayomzunguka hali hii itasaidia kuimarishwa usafi na hivyo kila mtu
anapaswa awajibike kwa uchafu anaouzalisha nyumbani kwake au sehemu ya
kazi yake kwani jukumu la usafi ni la kila mtu” alisisitiza . Samataba.
Alisema kuwa kila Halmashauri nchini inapaswa kujipanga
vizuri katika kuhakikisha kuwa inaondoa uchafu mitaani na kusafisha
maeneo yake ili kuondokana na tatizo la kipindupindu.
Samataba aliwaagiza viongozi wa Manispaa ya Temeke na
Halmashauri nyingine nchini kusimamia suala la usafi kuhakikisha
linakuwa endelevu kwani jukumu la usimamizi wa usafi ni la kila mtu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya
Temeke Photidas Kagimbo alisema kuwa wananchi wa Halamashauri hiyo
wamelipokea suala la utekelezaji wa agizo la Rais na wanaahidi
kuhakikisha kuwa maeneo yote yanakuwa safi siku zote.
0 comments :
Post a Comment