Aliyekuwa
mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na kuungwa mkono na vyama vya
upinzani vinavyounda Ukawa, Edward Lowassa amewakumbusha Wabunge na
Mameya wa chama hicho ambao watashindwa kutekeleza vizuri majukumu yao
kuwa watafukuzwa katika chama hicho.
Ikumbukwe kuwa kitendo cha kutimuliwa uanachama kinaweza kupelekea mbunge au Meya kupoteza nafasi yake moja kwa moja.
Lowassa
alikumbusha tahadhari hiyo jana alipokutana na Mameya na Manaibu Meya
wa Ukawa walioshinda katika Manispaa za Kinondoni na Ilala jijini Dar es
Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani kushika nafasi
hiyo tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.
Waziri
Mkuu huyo wa zamani aliwapongeza viongozi hao wapya na kuwataka kufanya
kazi kubwa ili kuwaonesha wananchi kuwa hawakukosea kuchagua Ukawa na
waone tofauti ya maendeleo kati ya vyama hivyo vya upinzani na CCM.
“Hili
ni agizo la Kamati Kuu (Chadema) kwamba mbunge na hata Meya wakishindwa
ku-perform, ikipita mwaka mmoja au miwili hawajafanya chochote
watafukuzwa kwenye chama,” alisema Lowassa.
Aliwataka
viongozi hao kuhakikisha wanafanya kazi kubwa ya kuliweka jiji la Dar
es Salaam kuwa safi na kutatua matatizo ya usafiri kwa wananchi.
Kadhalika,
aliwataka viongozi hao kukusanya mapato kuliko wakati mwingine wowote.
Pia, kutoogopa kukopa katika mabenki ili waanzishe miradi endelevu
itakayowagusa wananchi moja kwa moja.
Mwanasiasa
huyo mkongwe pia aliwataka Mameya na Manaibu Meya hao kuhakikisha
wanakubaliana na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) kuwa hawataingiliwa na kuzuiwa na Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa
Wilaya katika kutekeleza majukumu yao.
“Muondokane na sheria inayowazuia kukopa benki, kopeni benki na chagueni miradi ambayo inawagusa wananchi,” Lowassa alieleza.
Kwa
upande wa Mameya na Manaibu Meya hao, walimshukuru Lowassa kwa jinsi
alivyowasaidia kushinda ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo na kuwajenga
kusaikolojia.


0 comments :
Post a Comment