Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akisaini kitabu
cha wageni katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma kabla ya kuanza ziara
ya kukagua miundombinu ya usafirishaji
umeme, miradi ya umeme vijijini
pamoja na shughuli za uchimbaji wa madini mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa
mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa.
Naibu Waziri
wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (wa kwanza kulia)
akizungumza na Meneja Mradi Ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme katika
mradi wa Miundombinu ya Usafirishaji Umeme wa Kilovolti 400 kutoka
Iringa hadi Shinyanga, Mhandisi James Mtei (katikati) mara baada kukagua
ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme kilichopo eneo la Zuzu mkoani
Dodoma.
Sehemu ya
mitambo katika kituo cha kupoozea umeme kilichopo eneo la Zuzu
mkoani Dodoma. Ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji mradi wa
ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme wa kilovolti 400 kutoka
Iringa hadi Shinyanga unaotarajiwa kukamilika mwezi Aprili mwaka huu.
Kituo kinajengwa na kampuni ya GSE&C na Hyosung kutoka Korea.(P.T)
Kampuni
ya Joti structures inayojenga miundombinu ya usafirishaji umeme wa
msongo wa kilovolti 400 kutoka Dodoma hadi Singida imetakiwa kukamilisha
ujenzi wa miundombinu hiyo ifikapo mwezi Aprili mwaka huu kama mkataba
unavyoelekeza.
Agizo
hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard
Kalemani wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani Dodoma ili kukagua
miundombinu ya usafirishaji umeme, miradi ya umeme vijijini pamoja na
shughuli za uchimbaji wa madini.
Alitoa
agizo hilo baada ya Meneja anayesimamia Mradi huo kutoka Shirika la
Umeme nchini (TANESCO), Mhandisi Oscar Kanyama kumueleza kuwa mkandarasi
huyo amekamilisha ujenzi wa nguzo (transmission tower) kwa asilimia 30
tu toka alipokabidhiwa kazi hiyo mwaka 2013.
“Mkandarasi
alianza kazi Novemba 2013 na anatakiwa akamilishe tarehe 20 Aprili 2016
na hadi kufikia Desemba mwaka 2015 ilibidi awe ameshaanza kuvuta nyaya
kutoka Dodoma hadi Singida lakini mpaka sasa hajaanza,” alisema Mhandisi
Kanyama.
Naibu
Waziri aliongeza kuwa mkandarasi huyo asipokamilisha kazi ndani ya muda
uliopangwa atalazimika kulipa gharama ambazo serikali itakuwa imeingia
kutokana na mkandarasi huyo kuchelewesha mradi husika na kupelekwa
mahakamani.
“Serikali
imeshalipa asilimia 60 ya gharama zinazotakiwa ili kukamilisha mradi
huu lakini huyu mkandarasi amekamilisha kazi kwa asilimia 30 tu, hii
haikubaliki, hatutamvumilia mtu yeyote anayekwamisha juhudi za
usambazaji umeme nchini, awe mkandarasi au wasimamizi kutoka serikalini
wanaosimamia miradi hii,” alisema Dkt. Kalemani.
Kwa
upande wake, Meneja Mkazi wa kampuni ya Joti Structures, D.N. Charjee
alimueleza Naibu Waziri kuwa watakamilisha kazi husika ndani ya muda
uliopangwa kama ilivyo ndani ya mkataba na kwamba asilimia 15 iliyobaki
ya vifaa vinavyohitajika ili kukamilisha kazi hiyo vitafika tarehe 12
Januari 2015.
- Wakati huohuo Naibu waziri amepiga marufuku shughuli za uchimbaji wa madini ya ujenzi ndani ya mita 30 kutoka katika korongo la Ihumwa mkoani Dodoma kwa kuwa zimekuwa zikiathiri uwepo wa maji katika kata ya Ihumwa na sehemu nyingine zinazotegemea maji hayo kwa shughuli mbalimbali.
Baada ya
kuona athari za uharibifu wa mazingira katika korongo hilo, Naibu Waziri
alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kati, Sostenes Massola
kuhakikisha kwamba agizo hilo linafanyiwa kazi kwani wananchi wengi
katika kata hiyo wanaopata kipato kutokana na kilimo cha umwagiliaji
wanaathirika.
“Sheria
ya mazingira hairuhusu kuharibu vyanzo vya maji, kama kuna uchimbaji wa
madini ya ujenzi , Kamishna Msaidizi lazima uhakikishe kwamba haufanyiki
ndani ya mita 30 kutoka kwenye mito na wachimbaji lazima wawe na
vibali,” alisema Dkt. Kalemani.


0 comments :
Post a Comment