Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka watendaji na wafanyakazi wote
wa Wakala wa ufundi na umeme (TEMESA), kufanya kazi kwa umoja, uwazi na
uadilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuhuisha ustawi wa wakala huo.
Akitoa mwelekeo wa utendaji wa
wakala huo wakati akizungumza na watendaji wa TEMESA Mhe.Prof. Mbarawa
amesema Serikali ya awamu ya tano inaitaka TEMESA kufanya kazi kwa
weledi ili kuongeza mapato na kuhudumia wateja wao kikamilifu ili
kuinua uchumi wa wakala huo na kuondoa malalamiko kwa wadau na
watumishi.
‘Acheni kufanya kazi kwa
upendeleo na usiri kwani huo ndio mwanzo wa hujuma na ubadhirifu hali
inayochochea malalamiko na kudumaza huduma za TEMESA’, amesema Prof.
Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameitaka TEMESA
kuhakikisha inatengeneza magari ya wadau wote kwa wakati na kutoa huduma
za vivuko kwa ufanisi na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kukuza
mapato na kuboresha huduma za ufundi na umeme.
Kwa upande wake Katibu mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sehemu ya ujenzi eng. Joseph
Nyamhanga ameitaka TEMESA kuongeza bidii Katika kukusanya madeni yake
ili ipate uwezo wa kibiashara na hivyo kumudu ushindani wa kibiashara.
Naye Mtendaji mkuu wa TEMESA Eng.
Marceline Magesa amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa TEMESA inaendelea
na mkakati wa kujenga vivuko vipya viwili ili kuongeza huduma hiyo
katika eneo la Magogoni jijini Dar es salaam na Pangani mkoani Tanga.
Aidha amemhakikishia Waziri kuwa
ukarabati wa vivuko unazingatiwa na uboreshaji wa karakana unaendelea
ili kuvutia wadau wengi kutengeneza magari yao katika karakana hizo.
Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA
ulianzishwa mwaka 2006 kwa lengo la kusimamia huduma za ufundi, umeme na
usimamizi wa vivuko ambapo hadi sasa takriban vivuko 28 vinasimamiwa na
wakala huo nchini kote.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
0 comments :
Post a Comment