CCM YATAKA MAALIM SEIF AKAMATWE NAKUWEKWA NDANI KWA MADAI HAYA HAPA




 



Wakati zikiwa zimebaki siku 21 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa marudio visiwani Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeibuka na hoja ya kutaka mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad, akamatawe na kuwekwa ndani kwa madai ya kujitangazia ushindi kinyume cha sheria.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar jana, Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar,  Waride Bakar Jabu, alisema Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, anapaswa kukamatwa na Jeshi la Polisi na kufunguliwa mashitaka ya kujitangaza mshindi wa urais wa visiwa hivyo baada ya uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 kabla ya kufutwa siku tatu baadaye na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.

Kabla ya Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi Oktoba 28, 2015, Maalim Seif aliwaambia waandishi wa habari kuwa matokeo rasmi waliyo nayo, na ambayo walikuwa wameyapata kutoka kwa mawakal wao katika vituo vyote vya uchaguzi visiwani humo, yalionyesha kuwa yeye anaongoza kwa kupata asilimia 52.87 ya kura zote na kumuacha mpinzani wake, Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, na hivyo akaitaka ZEC itende uadilifu kwa kutangaza mshindi halali wa uchaguzi huo.

Hata hivyo, akizungumza jana, Jabu alisema Maalim Seif alikiuka sheria za uchaguzi na hivyo anastahili kukamatwa na kufunguliwa mashitka yake.

“Kitendo cha Maalim Seif kujitokeza hadharani na kutangaza kuwa ameshinda  urais Oktoba 25 mwaka uliopita  kabla ya kura kuhakikiwa na kutangazwa na ZEC ambayo ndiyo yenye dhamana ni kinyume cha Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar na kingeweza kuleta mtafaruku wa kisiasa,” alisema Waride, aliyekuwa ameongozana na kiongozi mwingine wa juu katikaa idara yake, Moderine Castico.

Aidha, alisema CCM ingependa kuona watu wote walioshiriki kuvuruga uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 wanakamatwa na kufunguliwa mashitaka kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu.

Alieleza kuwa uchaguzi uliovurugika umeipa hasara kubwa serikali lakini inashangaza kwamba hakuna hata mtendaji mmoja aliyefikishwa mahakamani kwa kuhusika na kosa hilo Kuhusu wasiwasi wa kukwama kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kama vyama vinavyoshiriki vitashindwa kukamilisha masharti ya katiba baada ya CUF kususia uchaguzi wa marudio, Waride alisema vyama vinavyoshiriki visidharauliwe na wala hakuna haki ya kuvipuuza.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Omar Ali Shehe, alisema Maalim Seif hana kosa alilofanya kwa madai ya kutangaza mwelekeo wa matokeo kabla ya tume ya uchaguzi.

Alisema taarifa alizotangaza ni matokeo yaliyokusanywa na mawakala wake katika majimbo na ndiyo kazi yao kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

“Vyombo vya sheria vinatambua hakuwa na makosa kutangaza mwelekeo wa uchaguzi na kwamba, matokeo rasmi hutangazwa na tume ya uchaguzi,” alisema Shehe.

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai Zanzibar (DDCI), Salum Msangi, alisema jana kuwa uchunguzi wa jalada la Maalim Seif la kudaiwa kujitangaza mshindi umekamilika na kukabidhiwa Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, tangu mwaka jana.

Mbali na jalada la Maalim Seif, pia alisema majalada mengine ambayo hadi sasa yapo kwa DPP ni pamoja na watendaji wa ZEC waliohusika kuvuruga uchaguzi wa Oktoba 25.

Juhudi za kumpata DPP Ibrahim Mzee Ibrahim kujua mwenendo wa majalada aliyodai DDCI kuwa yamekamilika hazikufanikiwa baada ya simu

yake kuwa imezimwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment