Nkupamah media
Akizungumza na gazeti hili Kisiwani Pemba Kamishna Hamdan amewatoa hofu wananchi kuwa hakuna mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura ambaye hataweza kwenda kupiga kura tarehe 20 machi mwaka huu wakati wa uchaguzi wa marudio kutokana na sababu za vitisho .
Amesema kwamba tayari Jeshi la Polisi limeanza kutengeneza mazingira ambayo yatawaweza wananchi kila mmoja kuwa huru na kuhakikisha kuwa usalama wa nchi utaendelea kudumishwa .
Katika mazungumzo na gazaeti hili katika Makao Makuu wa Jeshi hilo Mkoa wa Kaskazini Pemba , Kamishna Hamdan amefahamisha hakuna mwananchi ambaye hatapiga kura kutokana na vitisho , labda aache kwa sababu zake mwenyewe .
“Hakuna mwananchi ambaye atapata fursa ya kupiga kura kwa sababu za vitisho , labda yeye asiende kwa sababu anazozijua yeye , lakini sio suala la vitisho ulinzi utaimarishwa maeneo yote ya Unguja na Pemba ”alisisitiza Hamdan .
Aidha Kamishna Hamdan amesema pamoja na kazi ya ulinzi wa wananchi na mali zao kuwa ni Polisi , lakini iko haja kwa wananchi nao kuwapa ushirikiano askari pindi wanapobaini kuwa viasharia vya vitisho au uvunjifu wa amani .
Ameeleza kwamba ni kazi ya Jeshi la Polisi kuona wanannchi wanaishi kwa amani katika nchi yao na wanafanya mambo kwa mujibu wa sheria , na kuongeza tayari changamoto zinazojitokeza ikiwemo vitisho wanazifahamu na wanazifanyia kazi ili zisilete athari wakati wa zoezi la uchaguzi .
“Niwahakikishie wananchi kwamba changamoto zinazojitokeza ikiwemo vitisho tunazifahamu , na tunashukuru wanazisema wazi wazi , labda niwahakikishie wananchi tumejipanga kuzikabili ili zisileta madhara kabla na baada ya uchaguzi huo ”alifahamisha .
Kamishna Hamdan pia ameeleza kwamba Jeshi limejipanga pia kubadilisha mfumo wa kusimamia ili changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi uliofanyika 25, oktoba mwaka jana wazigeuze kuwa fursa .
Akizungumza ulinzi katika maeneo ya Visiwa Vidogo vidogo , amesema kwamba watawatumia askari shehia kutoa taarifa ili waweze kuyafikia maeneo yote huku akisisitiza kwamba namba za simu za makanda wa Polisi Mikoa yote ziko wazi na zinafahamika na wananchi waliowengi .
“Sisi tupo wengi na maeneo yote tunayafahamu , kwa hili tutawatumia zaidi askari wetu wa shehia na kikubwa zaidi ni kwamba makamanda wote wa mikoa Zanzibar namba zao za simu ziko wazi muda wote wananchi wanatakiwa kuwapigia na kuwaeleza changamoto zinazowakabili ”alieleza.
Hata hivyo alisema kwamba Jeshi la Polisi litafanya kazi kwa karibu na Serikali za Shehia kwa kuwatumia masheha na kamati zao kuhakikisha taarifa zote za uvunjifu wa amani zinaripotia na zinachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria .


0 comments :
Post a Comment