Mwakilishi Maalum wa Umoja wa
Afrika (AU) katika mgogoro wa Libya, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete leo amekutana na Naibu Waziri wa
Mambo ya nje wa Italy Dk. Mario Giro, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu
ya CCM Lumumba jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya mazungumzo maalum.
Akizungumza na waandishi wa
habari baada ya mazungumzo, Msaidizi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa,
Suleyman Mwenda alisema, Dk. Kikwete amekuwa na mahusiano ya kirafiki ya
muda mrefu na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italy Dk. Mario Giro,
hivyo Naibu Waziri huyo amefanya ziara hiyo ikiwa ni sehemu ya kumjulia
hali kama rafiki yake wa muda mrefu.
“Pamoja na kuja kumsalimia kama
rafiki wa siku nyingi, lakini lengo hasa la Naibu waziri huyo ni kutaka
maelezo juu ya suala la Libya’ alisema Mwenda na kuongeza “Kama
mnavyofahamu kuwa Dk. Kikwete ameteuliwa na Jumuiya ya Afrika (AU) kuwa
mwakilishi katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Libya”.
Alisema, Italy inalipa umuhimu wa
kipekee suala la Libya kutokana na kwamba nchi hiyo ni jirani hivyo
ina maslahi mapana na ya karibu juu ya suala la amani ya Libya, Dk. Giro
ameiwakilisha nchi yake katika kujua hatua ya usuluhishi na hatma ya
mgogoro wa Libya.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri
huyo aliambatana na Balozi wa Italy hapa nchini, Luigi Scotto pamoja na
Dk. Raffaele De Lutio, Mkurugenzi wa Masuala ya Kimataifa wa Italy.
0 comments :
Post a Comment