Mahakama
ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyoko The Hague nchini Uholanzi
imefuta kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto na
mwandishi wa habari Joshua Arap Sang waliokuwa wakituhumiwa kuhusika
katika vurugu na mauaji ya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Majaji
wa ICC wameeleza kuwa wameamua kuiondoa kesi hiyo baada ya kuwepo kwa
mkanganyiko katika ushahidi uliofikishwa mahakamani.
Baadhi
ya mashahidi walianza kubadili ushahidi wao huku wengine wakijiondoa
kwa madai kuwa walishinikizwa au kushawishiwa kutoa ushahidi huo.
Katika
uamuzi wao, majaji hao wameeleza kuwa kuondolewa kwa kesi hiyo
hakuwazuii wawili hao kushtakiwa tena kwenye mahakama hiyo au mahakama
nyingine ya kimataifa na kitaifa.
Uamuzi
huo wa ICC umepokelewa kwa hisia tofauti nchini humo. Wapo
walioufurahia na kueleza kuwa kesi hiyo ilijaa mihemko ya kisiasa zaidi
na kwamba kwa kuachiwa huru Ruto atakuwa na nafasi nzuri zaidi ya
kuendelea kuwatumikia wananchi wake kwa umakini zaidi.
Lakini
wapo wanaolalamikia uamuzi huo wakiwaangazia hasa wahanga wa machafuko
hayo yaliyopelekea mauaji ya zaidi ya watu 1000 na kuwakosesha makazi
maelfu ya raia.
Waathirika
wa tukio hilo wanaonekana kuwa katika hali ya sintofahamu zaidi kwani
uamuzi wa mahakama hiyo haukufikia hatua ya kuweza kubainisha iwapo Ruto
na Sang walikuwa na hatia.
0 comments :
Post a Comment