DAR ES SALAAM: Staili inayotumiwa na Rais John Pombe Magufuli kuibuka
katika maeneo mbalimbali mitaani pasipo kutarajiwa, inaonekana kuwashtua
wengi huku wengine wakihoji juu ya usalama wake,
Wakizungumza kwa njia ya simu kutoka
maeneo mbalimbali nchini, wananchi wameonesha mshtuko wao, wakisema
staili hiyo inaweza kuwapa nafasi maadui zake, waliodai ni wengi, kuweza
kumdhuru kwa namna yoyote.
“Unajua utendaji kazi wa Magufuli
umempatia maadui wengi na bahati mbaya, wabaya wake ni watu wenye uwezo
wa kufanya lolote wakati wowote, sasa anapojitokeza katika maeneo ya
wazi bila ya kuwepo ulinzi wa kutosha inatutisha sana, wanaweza kumdhuru
hawa mafisadi,” alisema Theo Marson kutoka Arusha.
“Hii ibukaibuka yake uswahilini tuna
wasiwasi ipo siku wajanja wanaweza kumdhuru, tunamuomba aache, wananchi
tusingependa kuona jambo lolote baya linamtokea maana yeye ni mtu muhimu
sana kwa Tanzania tunayoitaka, mtusaidie kuziambia mamlaka
zinazohusika, ulinzi wake uimarishwe,” alisema Mary Jopel kutoka Mtwara.
Gazeti hili lilijaribu kuwasiliana na
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Grayson Msigwa ili kupata
ufafanuzi wa hofu hiyo ya wananchi, lakini baada ya kuomba aandikiwe
ujumbe mfupi kupitia simu yake, hakuweza kutoa majibu hadi gazeti hili
linakwenda mtamboni.
Tangu kuchaguliwa kwake, Rais Magufuli
ameshaibuka sehemu tatu pasipo kutegemewa. Mara ya kwanza ilikuwa ni
wakati alipotembelea ofisi za Hazina, akikatisha kwa miguu kutoka ikulu.
Pia aliibuka ghafla katika Soko la Kimataifa la Feri jijini Dar es
Salaam na kushirikiana na wananchi kufanya usafi.
Katika tukio la karibuni zaidi, wiki
iliyopita Rais Magufuli aliibuka katika Tawi la Benki ya CRDB, Holland
House, makutano ya mitaa ya Samora na Ohio, jijini Dar es Salaam akiwa
katika gari la kiraia bila msafara kama ilivyozoeleka.
CHANZO: globalpublishers.co.tz


0 comments :
Post a Comment