Meneja wa mradi wa Ujenzi wa Flow Meter
ya Kigamboni Eng. Mary Mhayaya akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa alipokagua maendeleo ya
ujenzi huo.
Muonekano wa Flow Meter mpya ya Kigamboni katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Muonekano wa Daraja la Kigamboni mara baada ya ujenzi wake kukamilika.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati) akijadiliana jambo na Mkuu
wa Kivuko cha Magogoni (kushoto) na Nahodha wa kivuko hicho (kulia)
wakati alipokikagua.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akipata maelekezo kwa Mkurugenzi
Msaidizi Barabara za Mijini Eng. Hussein Mativila (kushoto) alipokagua
Daraja la Kigamboni.
………………………………………………………………………………………………….
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema mtambo mpya wa kisasa wa
kupima mafuta yanayoingia nchini flow meter unaojengwa
Kigamboni jijini Dar es salaam uko katika hatua za mwisho za kukamilika
kwake na utaanza kazi rasmi mapema mwezi ujao.
Prof. Mbarawa amesema hayo wakati
alipokagua mtambo huo unaosimamiwa na Mamlaka ya Bandari nchini (TPA)
na kuhimiza waendeshaji wa mtambo huo wawe watu wenye uadilifu wa hali
ya juu na elimu ya kutosha ili kuulinda na kuwezesha kufanyakazi
inavyostahili.
“Hakikisheni mnawasiliana na
Wakala wa Vipimo nchini (WMA), ili wahakikishe mtambo huu unaviwango
vinavyotakiwa vitakavyowawezesha wafanyabiashara wa mafuta kuridhika na
ufanyakazi wa mtambo huu ili kuondoa malalamiko”, amesema Prof. Mbarawa.
Zaidi ya shilingi bilioni 12
zimetumika katika ujenzi wa mtambo huo ambao utawezesha Serikali kupata
mapato stahiki na wafanyabishara kupata mafuta sahihi kwa mujibu wa
mahitaji yao.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua ujenzi wa Daraja la Kigamboni na kuwataka wananchi
kuhakikisha wanalitumia daraja hilo kwa usahihi na kuepuka vitendo vyote
vya hujuma.
Amesema daraja hilo lililojengwa
kwa zaidi ya shilingi bilioni 214 linatarajiwa kufunguliwa rasmi Aprili
16 na litakuwa na njia sita za magari na mbili za watembea kwa miguu.
“Nawataka wananchi na watumiaji
wote wa daraja hili kuhakikisha kuwa miundombinu ya daraja haihujumiwi
na watu wenye nia mbaya kwani vitendo vya aina hiyo licha ya kuharibu
daraja vitahatarisha usalama wa watumiaji”, amesisitiza Waziri Prof.
Mbarawa.
Naye Msimamizi wa Daraja hilo
kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Eng. Karim Mataka
amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa Daraja la Kigamboni
umekamilika katika hatua zote na kinachosubitriwa na ufunguzi na kuanza
kutumika.
Amesema wamejipanga vizuri
kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kuhusu matumizi ya daraja hilo kwa
madereva na watembea kwa miguu ili kuepuka usumbufu siku za mwanzoni.
Daraja hilo litakalofunguliwa
rasmi Aprili 16 litapunguza msongamano wa usafiri kwa wakazi wa
kigamboni na maeneo ya katikati ya jiji la Dar es salaam.


0 comments :
Post a Comment