Wakati
Rais John Magufuli akitoa salamu za pole kwa wakazi wa jiji la Mwanza,
kutokana na mauaji ya watu watatu waliouawa kwa kukatwa mapanga wakiwa
msikitini, Baraza Kuu la Waislamu (Bakwata) limelaani mauaji hayo.
Aidha,
Baraza hilo limewataka waislamu kuwa watulivu na kutoa ushirikiano kwa
vyombo vya usalama ili wahalifu hao waweze kukamatwa na kufikishwa
katika vyombo vya sheria.
Kauli
hiyo imetolewa na Mufti na Shehe Mkuu Abubakari Zubeir wakati
akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mauaji hayo yaliyotokea
Jumatano saa mbili usiku wakati waumini hao wakifanya ibada.
Shehe
Zubeir alisema tukio hilo la watu wasiojulikana kuvamia na kuwaua
waumini msikitini ni la kinyama ambalo halipaswi kuvumiliwa.
“Kwa
niaba ya Bakwata tunalaani vikali tukio hili pamoja na kuwataka
waislamu kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu. Lakini pia nawaomba
Waislamu na wananchi kwa ujumla kuvipa ushirikiano vyombo vyetu vya
usalama ili wahalifu hawa wapatikane,” alisema Shehe Zubeir.
Alisema
Uislamu ni dini ambayo moja ya misingi yake ni kulinda nafasi kama
anavyosema Mwenyezi Mungu katika Kitabu Kitakatifu cha Quran na kuongeza
baraza hilo linawapa pole wafiwa wote pamoja na waumini wa Masjid
Rahmaan kwa msiba huo.
Aidha, alitoa agizo kwa Bakwata Mkoa wa Mwanza kufuatilia kwa karibu hali za majeruhi na wafiwa.
“Kama
ambavyo naawagiza Bakwata Mkoa wa Mwanza nawaomba pia taasisi
mbalimbali za Kiislamu pamoja na Waislamu na Watanzania kwa ujumla kuwa
tayari katika kusaidia familia za wafiwa kwani wanahitaji kufarijiwa na
kusaidiwa,” alisema.
Blogger Comment
Facebook Comment