TUHUMA za ubadhirifu wa Sh bilioni 1.4 za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, zilizotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma, zimefikishwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Mkuu
wa Wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga, alisema Takukuru inakamilisha
uchunguzi wa kina ili wahusika waliofanya ubadhirifu huo wachukuliwe
hatua za kisheria.
Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Alisema upo ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliofanywa na wahusika waliopewa dhamana ya kusimamia matumizi yake.
Ngaga
alisema, ofisi yake baada ya kuunda tume ndogo na kubaini hilo,
uchunguzi wa awali unaonesha Sh milioni 513 zimefanyiwa ubadhirifu .
Alisema,
aliona ni vyema achukue hatua ya kukabidhi tuhuma hizo kwa Takukuru
wafanye uchunguzi wa kina kutambua ni nani aliyehusika na ubadhirifu
huo.
Alisema, taarifa na majina ya wahusika waliofanya hivyo itatolewa baadaye Takukuru ikikamilisha kazi yake.
“Takukuru
inaendelea na uchunguzi, ikikamilisha taarifa itatolewa. Katika maelezo
yangu ya awali kwenye Baraza la Madiwani lililokaa juzi sikuhukumu mtu
wala kusema amehusika, hivyo tusubiri tutajulishwa,” alisema.
Aliongeza
kuwa, uchunguzi huo utakapokamilika, taarifa husika zitapelekwa kwa
Mwenyekiti wa Baraza la Ulinzi na Usalama mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu
awasilishe kwa Waziri mwenye dhamana.
Awali,
tuhuma za ubadhirifu huo, zilitolewa na Mkuu wa Wilaya kwenye kikao cha
Baraza la Madiwani wa wilaya hiyo, Mei 11, mwaka huu.
Blogger Comment
Facebook Comment