RUFANI
ya Jamhuri kupinga hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro
kumwachia huru Sheikh Ponda Issa Ponda, dhidi ya kosa la kushawishi
wakazi wa mkoa huo kufanya kosa, ilikwama kuendelea jana na kuahirishwa
kwa wiki tatu baada ya mawakili wa utetezi kuomba muda wa kujadili na
mteja wao.
Jana kesi hiyo ilitajwa na Jaji Edson Mkasimongwa katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Wakili
wa Serikali Malangwe Mchungahela alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa
kutajwa jana kwa ajili ya kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza.
Hata
hivyo, mawakili wa utetezi, Abubakar Mohammed na Juma Nassoro, kwa
nyakati tofauti waliomba mahakama kuwapa muda wa kuzungumza na Sheikh
Ponda, kama wataendelea kutoa huduma kwake ama la.
Nassoro alidai
kuwa makubaliano yao ya awali ya kumtetea katika mahakama ya chini
yalishamalizika, na hakuna maelekezo yoyote ili kuweza kumuwakilisha
mahakamani hapo. Jaji Mkasimongwa alisema kesi hiyo itasikilizwa Julai 23.
Katika
rufani hiyo, upande wa Jamhuri uliwasilisha hoja nne ikiwemo, mahakama
ya chini ilikosea kwa kutokuzingatia uzito wa ushahidi wa kielektroniki
katika kutoka uamuzi wake.
Sababu ya pili na ya tatu, Jamhuri
inadai, Hakimu wa Mary Moyo alikosea aliposema hati ya mashtaka ilikuwa
na mapungufu ya kisheria na Sheikh Ponda hakuwa na nia ya kushawishi
umma wa mkoa huo kufanya kosa siku ya tukio.
Sababu ya mwisho ya
Jamhuri katika kupinga kuachiwa huru kwa Sheikh Ponda ni kwamba hakimu
alikosea kusema kuwa ilishindwa kuthibitisha kosa bila kuacha shaka.



Blogger Comment
Facebook Comment