Mamia ya wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh wameangamizwa katika operesheni za kulisafisha eneo la al-Khalidiyyah mkoani al-Anbar nchini Iraq.
Katibu wa Taasisi ya Badr nchini Iraq, Hadi Al-Amiri ametangaza kuwa, katika operesheni za kukisafisha kisiwa hicho kilichokuwa kinakaliwa na wanachama wa genge la Daesh, zaidi ya magaidi 1000 wameangamizwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, katika operesheni hizo, harakati za wananchi za kujitolea zinazofahamika kama Hashd al-Shaab imewatia mbaroni makumi ya magaidi wa kundi hilo.
Habari nyingine zinaeleza kuwa harakati za wananchi zimefanikiwa kuharibu ndege moja isiyo na rubani iliyokuwa inamilikiwa na wanachama wa Daesh katika mji wa Bayji, ulioko mkoani Saladin, kaskazini mwa nchi hiyo.
Tangu mwezi mmoja uliopita sanjari na operesheni za kuukomboa mji wa Fallujah kutoka mikononi mwa wanachama wa Daesh, jeshi la Iraq limekuwa likitekeleza operesheni kadhaa kaskazini mwa nchi hiyo na katika mkoa wa Saladin, ambapo hadi sasa limefanikiwa kudhibiti makumi ya vijiji na maeneo muhimu ya kusini mwa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi hao.
Wakati huo huo duru za habari mjini Mosul zimearifu kwamba, kundi la kigaidi la Daesh limepunguza idadi ya wapiganaji wake mjini hapo kwa zaidi ya asilimia 70. Kwa mujibu wa habari hiyo, kundi hilo limepunguza wapiganaji wake kutoka elfu 12 na kufikia elfu tatu na kwamba hali hiyo imetokana na uhaba mkubwa wa wanachama wake.
Ramani ya Iraq
Mmoja wa Makamanda wa kundi la kigaidi la Daesh, Kamanda Abu Wahib (Kushoto) akiwa katika moja ya mashambulizi katika mji wa Iraq. (AFP)
0 comments :
Post a Comment