Matokeo ya uchaguzi nchini Gabon yanatarajiwa kutoka siku ya leo Agosti 30, baada ya wananchi kupiga kura Agosti 27 mwaka 2016.
Matokeo hayo yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa baina ya vyama vikuu pinzani nchini humo vinavyoongozwa na Ali Bongo Ondimba wa chama cha Demokrasia cha Gabon -PDG na Jean Ping wa chama cha Vikosi vya Umoja wa mabadiliko – UFC.
Aidha kumekuwa na shutuma mbalimbali baina ya vyama hivyo tangu siku ya Jumamosi ambapo kila mmoja amemshutumu mwenzake kwa wizi wa kura na matumizi mabaya ya sheria na katiba.
Msemaji wa mgombea Urais kupitia  chama cha PDG Alain-Claude Bilie amemshutumu Bw.Jean Ping wa chama cha UFC kwa kuwavunjia heshima Taasisi ya Uchaguzi ya nchini humo kwa kuandaa na kuchapisha matokeo ya uongo ya chaguzi ndogo.
Lakini pia mkurugenzi wa kampeni za mgombea wa Urais kupitia chama cha UFC Bwana Jean Gaspard Ntoutoume nae amemtuhumu Bw.Ali Bongo wa chama cha PDG kwa kutumia Mahakama ya kikatiba kwa kufanya udanganyifu katika kura za huduma za usalama za nchini humo.
Ali Bongo anashindania nafasi hiyo ya Uraisi kwa mara pili baada ya kuchukua madaraka kutoka kwa baba yake Omar Bongo Ondimba mnamo mwaka 2009 baada ya kifo chake.
Gabon ni nchi ambayo inafanya uchaguzi kila baada ya ngwe ya miaka 7 na katika Uchaguzi wa mwaka huu wapo takribani wagombea 11 wanaoshindania nafasi hiyo ya uongozi nchini Gabon.
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC).