Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametoa maagizo
kwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Bodi ya Shirika la
Ndege la Tanzania (ATCL) kuwafukuza kazi pamoja na kuwachukulia hatua
wafanyakazi wa shirika hilo watakao kiuka mikataba yao na kuisababishia
hasara.
Rais
Magufuli ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua
ndege mbili mpya za serikali na kutia saini mkataba wa ukodishaji ndege
baina ya serikali na ATCL.
Dk.
Magufuli amesema serikali itaikodisha ndege hizo ATCL ambapo itailipa
serikali sehemu ya mapato yake, ili iache kuitegemea serikali katika
uendeshaji wake pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
“Tutawakodisha
ndege ATCL ili waache kufanya kazi kwa mazoea, ninaitaka kufungua
akaunti maalumu ya fedha benki ili kuweka mapato yatakayopatikana pindi
ndege hizo zitakapoanza kufanya kazi, na kama mapato yatakuwa mazuri
tutaiachia ndege hizo na kisha serikali kununua ndege nyengine, ”
amesema.
Ameitaka ATCL kudhibiti mianya ya rushwa, ukwepaji kodi na ufujaji wa mali za shirika hilo ili lisijiendeshe kwa hasara.
“ATCL
mkajipange vizuri katika upangaji wa ruti, bodi msiruhusu mtu kusafiri
bure, hata mimi nikija mnitoze nauli, hata Waziri Mbarawa akija atozwe
nauli, hivyo ndivyo biashara inakwenda, mwisho wa siku mtapimwa kwa
utendaji kazi wenu, mtakapo haribu kazi hao viongozi hawatakuja
kuwatetea, ” amesema.
Ametoa
onyo kwa wafanyakazi wasio na uwezo wa kufanya kazi katika shirika hilo
kuacha kazi kabla hawajatumbuliwa na kwamba serikali iko tayari kulipa
fidia zao pindi watakapofanya hivyo.
“Wale waliojipanga kwenda na mwendo huu tutakwenda nao, wanaohisi hawezi kwenda na kasi hii waachie ngazi tutawapa malipo yao, “
Aidha ameitaka bodi ya ATCL kutoa huduma nzuri na kuzingatia ratiba ili kushindana katika soko la usafiri wa anga.
“Ndege
mmezipata, mkizitumia vibaya hazitatufikisha popote. Mnaingia kwenye
ushindani wa kweli. Ukitaka kukuza uchumi na sekta ya utalii lazima uwe
na ndege inayofanya kazi vizuri, ” amesema.
Amesema ndege hizo zitasaidia wananchi wa vipato vya chini kwa kuwa zinauwezo wa kutua kiwanja chochote.
“Ndege
hii inatua popote wananchi wa Dodoma, Songea, Mtwara, Musoma, Kigoma,
Mafia na Zanzibar watanufaika na usafiri huu, ” amesema.
Mwenyekiti
wa Bodi ya ATCL, Emmanuel Korosso ameishukuru serikali kwa kulifufua
shirika hilo na kuadi kuzitunza ndege hizo mpya ili zidumu kwa muda
mrefu pamoja na kuiletea faida serikali.
Na Regina Mkonde


0 comments :
Post a Comment