Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora leo imeadhimisha miaka 50 ya kuzaliwa kwake jijini Dar es Salaam, kwa kutoa tuzo za uwajibikaji na utawala bora kwa familia ya muasisi wa Taifa hili na aliyekuwa rais wa awamu ya kwanza Hayati Julias Kambarage Nyerere na Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Alhaji Ally Hassan Mwinyi.
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bahame Nyanduga, wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki akiikabidhi tuzo ya Mwl. Nyerere kwa mjukuu wake Moringe Nyerere, amesema tume hiyo itaendelea kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kuwa ndiyo muasisi wa tume hiyo, vilevile aliacha msingi mzuri wa utawala bora na haki za binadamu nchini.
“Tuzo hii imetolewa kwa familia ya Mwl. Nyerere kutokana na kazi nzuri aliyofanya ya kukuza haki za binadamu na utawala bora nchini, pia ndiye muasisi wa tume hii,” amesema.
Nyanduga amesema kuwa, tuzo ya pili imetolewa kwa rais mstaafu Mwinyi kutokana na mchango wake katika kusimamia misingi ya haki za binadamu na utawala bora enzi za utawala wake.
“Rais Mwinyi aliwajibika, alijituma, na kuhakikisha watumishi wa umma wanatekeleza majukumu yao kwa misingi ya utawala bora kwa kuzingatia matakwa ya sheria, katiba na kanuni,” amesema.