Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh.Mwigulu Nchemba, ameombwa kuchukua hatua dhidi ya polisi mkoani Kigoma kufuatia kifo chenye utata cha kijana Hussein Badru Gwemera, mwenye umri wa miaka 25, mkazi wa Majengo, ambaye inadaiwa amefariki kutokana na kupigwa na askari polisi.
Marehemu na wenzake wanne walikamatwa na askari polisi usiku wa Jumapili iliyopita katika eneo la stendi kuu ya mabasi mjini Kigoma wakituhumiwa kwa wizi wa milango ya mtu ambaye hata hivyo hajafahamika na kupelekwa kituo kikuu cha polisi kati.
Ndugu wa marehemu akiwemo baba yake mzazi Badru Gwemera, wamesema hawakuwa na taarifa za kukamatwa kwa mwanae, mpaka alipopata taarifa za kifo chake siku ya Jumanne na kuambiwa kuwa mwili wa marehemu ulikuwa chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya mkoa, Maweni.
Amesema kuwa baada ya kufika katika chumba cha kuhifadhia maiti walibaini kuwa marehemu amepigwa mpaka kuvunjwa mkono wake wa kushoto na kung’olewa jino na kwamba daktari aliwathibitishia kuwa marehemu kabla ya kifo chake alipigwa
Amesema baada ya kutoridhishwa na mazingira ya kifo cha mwanae, waliamua kwenda ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kigoma, ili kuomba msaada zaidi, lakini hata hivyo hawakufanikiwa badala yake walikamatwa na askari polisi.
Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, limetoa maelezo yanayokinzana kwani hapo awali kaimu kamanda wa polisi ACP Obadia Nselu, amekaririwa akisema hakuwa na taarifa za tukio hilo kabla hapo baadaye kueleza kuwa marehemu alifariki wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Maweni baada kuanguka ghafla akiwa mahabusu.
Hata hivyo kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa wa Kigoma, Maweni, Dr.Juma Masanja Msengeli, ambaye ameongea kwa sharti la kutorekodiwa, alisema hakuna taarifa yoyote inayoonyesha kuwa kabla ya kufariki marehemu alipatiwa matibabu hospitalini hapo,
Amesema siku ya Jumatatu ya Octoba 17 askari polisi walifika hospitalini hapo na mwili wa marehemu na kwenda moja kwa moja mpaka katika chumba cha kuhifadhia maiti, ambapo walipokelewa na mhudumu ajulikanae kwa jina la Mangalala kisha baadaye mwili wa marehemu kufanyiwa uchunguzi.
Aidha kwa mujibu wa kibali cha mazishi kilichoandikwa na mkuu wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Maweni, Dk. Hoseah aliyefanya uchunguzi wa mwili wa marehemu kinaonyesha kuwa marehemu huenda alifariki kutokana na kupigwa (Probably Traumatic Injury), kilisomeka hivo.
Tukio hilo limegusa na kusikitisha watu wengi ambapo baadhi ya waombolezaji walisikika wakisema kuwa vyombo vya juu vya serikali vichukue hatua dhidi ya askari watakaobainika kuhusika na kifo hicho ili haki iweze kutendeka.
Na Mwandishi wetu,Kigoma