Licha
ya baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa Chama cha Wananchi (CUF) na wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kutamka kutomtambua Profesa Ibrahim
Lipumba kama mwenyekiti wa CUF.
Lipumba
ameendelea kufanya shughuli za chama hicho ambapo leo ameteua
wakurugenzi wapya kwa madai ya kujaza nafasi za wakurugenzi alizotengua
teuzi zao jana.
Miongoni
mwa Wakurugenzi aliodai Lipumba kuwateua ni pamoja na Mkurugenzi wa
Uchumi na Fedha Thomas Malima, Maftaha Nachuma aliyedai kumteua kuwa
Mkurugenzi wa Mambo wa Nje CUF, Zaynab Mndolwa kuwa Mkurugenzi wa Haki
za Binadamu pamoja na Jaffari Mneke kuwa Mkurugenzi wa Mipango na
Uchaguzi.
Hata
hivyo, Lipumba amedai kuwa, aliowateua watakaimu nyadhifa hizo baada ya
kuthibitishwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la CUF.
Aidha, amedai kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje atamteua kutoka Zanzibar hapo baadae.
Sambamba
na hilo, amesema wakurugenzi na manaibu wakurugenzi aliowateua baada ya
mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Juni, 21, 2014 wataendelea na
nyadhifa zao huku akitishia kuwa, ikimbidi kufanya mabadiliko ya
wakurugenzi hao hatosita kufanya hivyo.
Katika
hatua nyengine, Lipumba amedai kutoa maagizo kwa Mkurugenzi wa Uchumi
na Fedha CUF ambaye ndiye Katibu wa Bodi ya Wadhamini kuitisha kikao cha
bodi hiyo Oktoba 4,2016 ili ipewe taarifa ya msimamo na ushauri wa
Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi kuhusu mgogoro wa
uongozi kitaifa wa CUF.
Lipumba
amesema kuwa, amefanya teuzi za wakurugenzi hao kwa mujibu wa katiba ya
CUF ya mwaka 1992 toleo la 2014 ibara ya 90 (1) (f) ambayo inasema kuwa
Mwwenyekiti Taifa atateua Wakurugenzi na Manaibu Wakurugenzi kutoka
miongoni mwa wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa au wanachama
jasiri wa chama.
Na Regina Mkonde


0 comments :
Post a Comment