BAADA ya Serikali kuzifungia timu za Simba na Yanga kutumia Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kwa muda usiojulikana kutokana na uharibifu wa
miundombinu uliofanywa na mashabiki wa timu hizo katika mchezo wa Oktoba
1 mwaka huu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limezitaka timu hizo
kuutumia Uwanja wa Uhuru.
Akizungumza na BINGWA jana, Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Tanzania
(TPLB), Boniface Wambura, alisema tayari wameshazijulisha timu hizo juu
ya kuutumia uwanja huo ili kuziondolea mzigo wa kuendelea kutafuta
sehemu ya kwenda kuchezea michezo yao.
“Tayari tumeshazitaarifu timu hizo kurudi kwenye Uwanja wa Uhuru
licha ya kuwa una kasoro kidogo iliyopelekea ziukimbie na kuomba
kuutumia ule wa Taifa, kimsingi timu hizi hazina viwanja na wakati
Serikali ikiwa bado inaendelea na msimamo wake wa kuufungia zitakuwa
zinautumia huu kwenye michezo yake inayoendelea,” alisema Wambura.
TFF ilizihamishia timu hizo Uwanja wa Taifa baada ya klabu ya Simba
kuhofia usalama wa afya ya wachezaji wake kutokana na plastiki
zinazoshika nyasi katika Uwanja wa Uhuru kuwaumiza katika michezo yake
mitatu iliyochezea hapo.
Sababu nyingine ambayo Simba ililalamikia ni uwanja kuwa mdogo,
ikitolea mfano mchezo wa Azam ambao ulipigwa dimbani hapo na baadhi ya
mashabiki wake walishindwa kushuhudia.
Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara, alipotafutwa kuzungumzia suala la
kurejea kwenye uwanja huo alisema kuwa viongozi watakutana kulijadili
suala hilo kwa sababu ni wao walioomba kuondoka hapo na kuhamishiwa
Uwanja wa Taifa.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Baraka Deusderit, alisema wao hawana
matatizo na kurudi kwenye uwanja huo kwa sababu walioomba kuondoka hapo
ni Simba na walikuwa na malengo ya kuomba kuutumia katika michezo yake
hata kabla ya Bodi ya Ligi kuwaruhusu kuutumia.


0 comments :
Post a Comment