Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli akiwa anatoka kwenye Wodi
ya Sewahaji katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kurejea nyumbani
mara baada ya kuruhusiwa baada ya kupata nafuu. Mama Janeth Magufuli
alikuwa amelazwa hospitalini hapo tangu tarehe 9 Novemba 2016.
………………………………………………………………………
Na.Alex Mathias.
Katika
kipindi cha mwaka mmoja ambao serikali ya awamu ya tano chini ya mhe,
Dr. John Pombe Magufuli imekaa madarakani, kuna mengi yaliyofanyika au
yaliyowekewa mipango ya kufanyika hapo mbeleni na wananchi wengi
kuonyesha kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa kwa ujumla
wake.
Moja
kati ya mambo ambayo yamewafanya wananchi wengi kufurahia na kujenga
imani juu ya serikali ni uboreshaji wa hospitali ya rufaa ya Muhimbili
ambayo imekuwa ni moja kati ya kero kubwa kwa miongo mingi na ilionekana
kama vile ni jambo lisilowezekana kutatua kero hiyo.
Zipo
kero ambazo zilihitaji serikali kuingilia kati kwakuwa ziligusa bajeti
kuu kwa mfano upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, fedha kwa ajili ya
utafiti wa magonjwa mbalimbali na hata maslahi ya waganga na wauguzi pamoja na wafanyakazi wote wa taasisi hiyo ya afya.
Itakumbukwa
kuwa kulikuwa na sakata la mashine za “MRI” na CIT Scan hii ikiwa ni
siku chache tu baada ya Mhe, Rais kuingia madarakani, kama haitoshi
suala la ununuzi na ufungaji wa
vitanda katika hospitali hiyo kutokana na fedha zilizokuwa zitumike
kwenye tafrija ya ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
ni baadhi ya hatua za mapema zilizochukuliwa kuboresha hospitali hiyo.
Lakini
ni ukweli usiopingika kwamba vipo baadhi ya vitu ambavyo havihitaji
serikali kuingilia kati ni suala la ubunifu na usimamizi wa uongozi wa
hospitali hiyo na kila mmoja kutimiza majukumu yake katika kulijenga
taifa kupitia maeneo yetu ya uwajibikaji.
Juma
lililopita mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth
Magufuli alilazwa katika hospitali hiyo ya Rufaa na ilikuwa ni moja
kati ya masuala yaliyogonga vichwa vya habari hapa nchini na kuzua
mijadala mbalimbali ikiwemo kutozoeleka kwa viongozi wetu na familia zao
kutibiwa katika hospitali za umma hapa nchini.
Lakini
ninachotaka kukijadili hapa siyo suala la Mama Janeth kulazwa katika
hospitali ya Rufaa Muhimbili, bali ni kile nilichokiona katika picha
wakati Mama Janet Magufuli akitoka wodini baada ya kuruhusiwa kutoka
hospitalini hapo ilinipa maswali mengi na muhimu yanayoanzisha majadala
juu ya hatima yetu kama taifa kuufikia ustawi wetu.
Ukiangalia
kwa makini katika picha ile inaonesha baadhi ya maeneo kama
milango,madirisha, samani nk vikiwa vimeharibika bila ya kufanyiwa
ukarabati wowote na hili linaleta shaka juu ya nani anapaswa kusimamia?
Je! uongozi wa Muhimbili haujaona kama sisi wengine tunavyoona katika
hii picha ? Au, hili nalo linahitaji Mhe, Rais na Waziri Mkuu ama
Mawaziri wa wizara husika waingilie kati?
Hili
ni suala ambalo halihitaji fedha za kigeni wala uchumi wa kati kwa
kuwa ninaamini kipo kitengo cha ukarabati ambacho kina wafanyakazi
wanaolipwa mshahara na serikali tena kuna wasimamizi walio juu yao ambao
haya wanapaswa kuyaona na kuyafanyia kazi bila ya kuhitaji kusukumwa.
Kinachohitajika
ni moyo wa kizalendo na kujituma huku tukiwa na mawazo ya kuijenga nchi
yetu kwa kufanya tunayopaswa kufanya bila ya kuwa na shinikizo kutoka
kwa walio juu yetu au manung’uniko kutoka kwa watumiaji wa huduma zetu,
na hiyo itakuwa ni ishara ya kupenda tunachokifanya na zaidi kuipenda
nchi nchi yetu.
Ili
taifa lolote liweze kujengwa na kukua hadi kufikia malengo yaliyowekwa
kunahitajika kuwe na moyo wa kujituma lakini pia kuwa na moyo wa
kutimiza wajibu kila mtu mahali pake pa kazi pamoja na ubunifu huku
kila mmoja akichukulia yote kama sehemu ya maisha yetu ya kila siku.
Hospitali
ya taifa ya Muhimbili licha ya kuwa ni hospitali ya Rufaa lakini pia
inatarajiwa kuwa mfano kwa hospitali zote nchini kwakuwa hii ndiyo kioo
cha afya na utendaji wa viongozi katika sekta hiyo muhimu katika taifa
letu. Hatupaswi kabisa kupuuzia hata kitu kidogo tu chenye viashiria vya
uzembe kwakuwa chanzo cha madhara yoyote kwa kiasi kikubwa huwa ni
uzembe.
Hapa kiukweli Uongozi wa
Muhimbili haujawajibika vya kutosha kwani vitu vidogo kama hivi ambavyo
vinatakiwa kukarabatiwa tu navyo mpaka Mh.Rais Dk. John Pombe Magufuli
aje ?Mimi naamini kwamba kazi ya kuitunza Hospitali ya muhimbili kwa
masuala ya ukarabati mdogomdogo sio jukumu la Serikali kuu bali ni
Uongozi wa Hospitali hiyo.
Uongozi
wa taasisi hii unapaswa kuliangalia hili kwa makini ili lisije
likaharibu taswira ya mambo mema wanayoyafanya madaktari na watumishi
wengine , lakini pia lisije likawa chanzo cha kuondoa uaminifu na weledi
wao katika mambo mbalimbali wanayokusudia kuyafanya. Wakumbuke tu kwamba “Hiari Yashinda Utumwa”


0 comments :
Post a Comment