Licha ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuwataka mawakili wake wasijihusishe na chochote baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kufuta rufaa yake, mawakili hao wamepeleka maombi kuiomba mahakama hiyo kumpa mteja wao muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata rufaa.
Kutokana na hali hiyo, Lema anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo ili kujua hatima ya maombi ya rufaa yake.
Desemba 2, mwaka huu, mahakama hiyo ilifuta rufaa ya mbunge huyo kutokana na kukatwa nje ya muda, huku mawakili wake wakitakiwa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ndani ya siku 10.
Hatua hiyo ilikuja baada ya uamuzi wa maombi ya marejeo ya mwenendo na uamuzi wa mahakama ya chini kutupwa na Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Sekela Moshi, Novemba 11, mwaka huu.
Wakili wa Lema, Sheck Mfinanga, jana alisema wamepeleka maombi mahakamani hapo wakiiomba impe mteja wao muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata rufaa na kusikiliza rufaa hiyo ya maombi ya dhamana.
“Tumepeleka maombi mahakamani ili impe Lema muda wa kupeleka notisi ya kusudio la kukata rufaa na kusikiliza rufaa yake. Maombi hayo yanatarajiwa kusikilizwa na Jaji Dk. Modesta Opiyo,” alisema Mfinanga.
Lema ambaye anashikiliwa kwa zaidi ya mwezi mmoja katika Gereza Kuu la Kisongo, mjini Arusha, alikamatwa Novemba 2, mwaka huu, nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani mjini Arusha, Novemba 8, mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka ya uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli.
Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Angero Rumisha, alisema mahakama hiyo imeifuta rufaa hiyo kwa sababu wakata rufaa waliikata nje ya muda.
Kutokana na sababu hizo, mahakama hiyo ilikubaliana na pingamizi la awali lililowasilishwa na mawakili wa Serikali, Paul Kadushi na Matenus Marandu, walioomba mahakama hiyo isisikilize rufaa hiyo kwa sababu imekiuka matakwa ya sheria, yanayotaka kutolewa kwa kusudio la kukata rufaa kabla ya rufaa yenyewe.
Novemba 28, mwaka huu, rufaa hiyo ilipangwa kusikilizwa kwa Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Fatuma Masengi, lakini ilishindikana baada ya mawakili wa Serikali kuweka pingamizi.
Kwa mujibu wa mawakili hao, mawakili wa Lema walikuwa wamekiuka matakwa ya sheria yanayowataka kutoa notisi ya nia ya kukata rufaa badala ya kukata rufaa yenyewe.
Katika shauri hilo, Lema anawakilishwa na mawakili Adam Jabir, John Mallya, Sheck Mfinanga na Faraji Mangula wakati upande wa Jamhuri unawakilishwa na Kadushi na Marandu.
0 comments :
Post a Comment